Wednesday, March 16, 2011

BASATA KUSUKA UPYA MASHINDANO YA UREMBOBaraza la Sanaa la Taifa litayafanyia mabadiliko makubwa mashindano yote ya urembo nchini ili yafanyike kwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo lakini pia kufanyika katika misingi ya haki na uwazi kuliko ilivyo sasa ambapo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya washiriki na wadau mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu barazani hapo wakati akihitimisha mada ya Mchango wa Mashindano ya Urembo na Mitindo katika Kukuza Ajira iliyokuwa ikiwasilishwa na Juliana Urio ambaye ni muandaaji wa Shindano la Kisura linalofanyika kila mwaka.
Alisema kwamba,Baraza linakusudia kuwaita waandaaji wote wa mashindano ya urembo na mitindo ili kuwakutanisha na wadau mbalimbali kwa ajili ya kueleza changamoto zilizopo na baadaye kuja na mapendekezo ambayo yatafanya mashindano hayo kuwa bora zaidi na yatakayofanyika katika misingi ya uwazi na haki zaidi.
“Tunatambua mchango wa mashindano haya lakini lazima yafanyike katika misingi iliyo wazi na bora zaidi ndiyo maana tunataka tuwaite waandaaji wote tuwakutanishe na wadau mbalimbali ili tupate changamoto na michango mbalimbali ya uboreshaji” alisema Materego.
Aliongeza kwamba, si nia ya Baraza kufuta shindano lolote lakini akasisitiza kwamba pale shindano linapokuwa na mapungufu mengi basi lazima lifutwe.Katika hili alisema kwamba, lazima waandaaji wazingatie masharti na taratibu zote wanazopewa ili kuepuka kufutwa kwa mashindano yao.
“Tunajua kwamba,ufutaji wa shindalo lolote utaathiri watu wengi hasa wasanii (warembo) sisi hatutaki kufika huko kwa sasa ndiyo maana tunasema mabadiliko katika uendeshaji wake ni ya msingi.Hatutaki mashindano ambayo washindi wanapatikana kwa misingi ya fedha na vigezo visivyostahili” alisisitiza Materego.
Kwa upande wake Juliana Urio alisema kwamba,washiriki wa shindano la kisura wamekuwa wakipatikana kutoka mikoa mbalimbali nchini na kusisitiza kwamba shindano lake limekuwa likifanyika katika misingi ya uwazi na haki kwani washindi wamekuwa wakipatikana kutokana na kura za wananchi na yeye kama muandaaji hajui kinachokuwa kinaendelea katika kumpata mshindi.
Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego (Kushoto) akisisitiza jambo kuhusu muenendo wa mashindano ya urembo nchini wakati akihitimisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye ukumbi wa baraza hilo.Wengine kutoka kulia ni Mratibu wa Jukwaa hilo,Ruyembe Mulimba na Juliana Urio muandaaji wa shindano la kisura.
Mmoja wa washiriki wa shindano la kisura akijibu baadhi ya hoja zilizoelekezwa kwa washiriki wa shindano hilo na wadau wa Jukwaa la Sanaa.Katikati anayemtazama ni Mshindi wa shindano la kisura anayemaliza Muda wake Diana.

No comments:

Post a Comment