b..

B1

Wynem

animation

Sunday, October 2, 2016

MAKAMU WA RAIS AZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM JANA

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka udongo katika mti alioupanda eneo la JKT Mgulani Barabara ya kilwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika jiji la Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliojitokeza katika eneo la JKT Mgulani ambapo shughuli za uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika jiji la Dar es Salaam zilifanyika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Mhe. January Makamba akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti iliyofanyika JKT Mgulani, barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam. 
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda akihutubia wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti jijini Dar es salaam inayokwenda kwa jina la MTI WANGU iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akijiunga na mtandao kwenye eneo la Gymkhana ambalo huduma ya WI-FI inapatikanika bure kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
...................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jana tarehe 1 Oktoba 2016 ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam katika uzinduzi rasmi wa kampeni ya upandaji miti inayojulikana kama Mti wangu Jijini Dar es Salaam.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo katika eneo la barabara ya Kilwa – Kurasini katika wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola mkoani Dar es Salaam ambavyo vimepewa jukumu la kutunza miti hiyo iliyopandwa ili isiharibiwe vihakikishe vinatekeleze jukumu ili kikamilifu ili kuhakikisha miti hiyo iliyopandwa inakuwa vizuri ili kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa miongoni mwa Majiji bora katika utunzaji wa Manzingira.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa kampeni hiyo ambayo ameizindua Jijini Dar es Salaam inatakiwa ifanyike nchini kote kama hatua ya kurejesha uoto wa asili na utunzaji wa vyanzo vya maji kote nchini.

Amesema kuwa jitihada za kupanda miti nchini zinatakiwa kuimarishwa maradufu kwani zitasaidia katika uhifadhi wa mazingira hususani katika suala zima la kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Makamu wa Rais katika hotuba yake ameeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuongezeka hewa ya ukaa katika jiji la Dar es Salaam kutokana na ongezeko la viwanda na idadi kuwa ya watu hivyo jitihada za pamoja kati ya serikali,taasisi binafsi,asasi za kiraia na wananchi zinahitajika katika kutunza mazingira na kupanda miti.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia amepongeza jitihada za uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam katika uboreshaji na uimarishaji wa mifumo ya maji katika barabara itakayosaidia kurahisisha umwagiliaji wa miti iliyopandwa.

Amesema anafaraja na matumaini makubwa kuwa kampeni aliyoizindua ya upandaji miti itakuwa endelevu na miaka michache ijayo italifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kivutio na mfano wa kuigwa na mikoa mingine kwa kuwa na mwonekano mpya na wa kuvutia.

Baada ya kuzindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais ambaye aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais Mazingira na Muungano January Makamba na Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe alifanya ziara fupi ya kutembelea na kukagua mifumo wa maji katika barabara ya Nyerere na Ally Hassan Mwinyi itakayotumika kumwagilia miti iliyopandwa pamoja na kuongeza na wananchi walioshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Gymkana.


PICHA ZAIDI BOFYA HAPA