Friday, March 25, 2011

BASATA: JENGENI NYUMBA SA SANAA WILYAYANIMoja ya michoro ya nyumba za asili za kabila la Wahaya zikionyweshwa kwa wadau wa sanaa.Muhadhili kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU),Dkt.C.Lwamayanga (kushoto) akiwapa elimu wadau wa Sanaa juu ya sanaa ya usanifu majengo kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii.W engine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idaya ya Mfuko na Uwezeshaji BASATA,Ruyembe C.Mulimba,Mkurugenzi wa Utamaduni anayeshughulikia Sanaa,Bi.Angela Ngowi na Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.
Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego (Kulia) akifafanua jambo mbele ya wadau wa Sanaa (hawako pichani) muda mfupi baada ya Dkt.Lwamayanga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi kumaliza kutoa mafunzo kwa wadau hao.
Wadau wakifuatilia mafunzo hayo.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mikakati ya kuandaa michoro maalum kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za sanaa katika ngazi za wilaya kwa kufuata tamaduni na desturi za ujenzi katika maeneo husika.
Mikakati hiyo ilitangazwa na Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego kwa wadau wa Sanaa mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ambapo alisema kwamba,zoezi hilo litafanyika kwa kuwashirikisha wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na lengo lake ni kuwa na mahali pa kuwakutanisha wasanii na kufanya maonyesho mbalimbali ya kazi zao katika ngazi mbalimbali.
“Tuko kwenye hatua nzuri ya kuandaa michoro ya majengo ya nyumba za sanaa katika ngazi za wilaya,tunakusudia kushirikiana kwa ukaribu na wataalam wenzetu kutoka Chuo cha Ardhi na tunategemea wenzetu huko wilayani watakuwa tayari kusukuma suala hili” alisema Materego.
Alisisitiza kwamba,awamu ya kwanza ya uchoraji ramani wa nyumba hizo za sanaa itakapokamilika,litaanza zoezi la ujenzi wa nyumba hizo ambazo zitakapokamilika zitakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya sanaa na utamaduni kwa ujumla hapa nchini.
Awali,Dtk.Lwamayanga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) aliwasilisha michoro ya ramani inayotumika katika kujenga nyumba za jamii mbalimbali nchini ambapo alisema kwamba,sanaa inayotumika katika kusanifu nyumba hizo za asili ni ya kiwango cha juu inayotakiwa kuenziwa na jamii kwa sasa.
Aidha,alikosoa dhana inayojengeka kwamba,usanifu majengo ni sayansi na kueleza kwamba ni sanaa ya ufundi ambayo inapaswa kutambuliwa katika tasnia na kwamba watu wanaochanganya dhana hii ni wale wasioelewa maana ya halisi ya sanaa na taaluma hiyo ya usanifu majengo.
“Hata wanafunzi wetu wamekuwa na tabu sana,ukiwaambia usanifu majengo ni sanaa wanakushangaa kwa kuwa awali walikuwa wanasoma Physics na Kemia basi wanaamini kwamba hata usanifu majengo ni sayansi pekee,hii si kweli kabisa,usanifu majengo ni sanaa na inapaswa kutambuliwa kwenye tasnia hii” alisisitiza Dtk.Lwamayanga.
Ama kwa upande mwingine aliwashauri wasanifu majengo kuzingatia asili ya makabila ya Tanzania katika kuchora michoro yao badala ya ilivyo sasa ambapo miji imepambwa na majengo yasiyowakilisha utamaduni wetu bali ule wa Ulaya.
“Tuna ramani nzuri sana za majengo kutoka kwenye makabila zaidi ya 125 yaliyoko nchini,tunaweza kuwa na majengo mazuri zaidi yenye mtizamo wa kitamaduni zaidi” alishauri Dkt.Lwamayanga ambaye ni Mhadhili na Mkuu wa Idara ya Usanifu Majengo Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).

No comments:

Post a Comment