Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ghonche Materego akikabidhi moja ya ngoma kwa Katibu wa Kundi la Nchabwede, Anna Said Nindimba kwenye hafla fupi iliyofanyika wiki hii kwenye ofisi za Baraza hilo.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey L. Mungereza akizijaribu ngoma hizo sambamba na Mwenyekiti wa Kundi la Nchabwede Bi. Ashinta.
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limekabidhi ngoma tatu za kisasa kwa Kikundi cha Ngoma za Asili cha Nchabwede katika kuamsha ari ya kukuza fani hiyo miongoni mwa wasanii.
Akikabidhi ngoma hizo kwenye Ofisi za BASATA kama sehemu ya kutekeleza ahadi aliyoitoa wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa, Katibu Mtendaji wa Barazahilo, Ghonche Materego amesema kuwa, ngoma hizo zimetolewa ili ziwe chachu kwa kundi hilo katika kufanya kazi zenye ubora na kuwapa hamasa ya kuendeleza fani hiyo.
“Tunawapa ngoma hizi tukiamini kuwa, zana hizi zimekuwa na changamoto kubwa. Mzitumie katika kuendeleza fani hii ya ngoma za asili na ziamshe ari ya kuirithisha kwa vijana” alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa, Baraza kwa muda mrefu limekuwa likiishauri na kuishawishi Serikali kupunguza ushuru kwenye vifaa vya Sanaa kama ilivyo kwenye zana za kilimo ili kuruhusu wasanii na wadau mbalimbali kununua vifaa hivyo kwa bei nafuu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza tasnia ya Sanaa.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi hicho chenye maskani yake Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, Anna Said Nindimba alishukuru kwa msaada wa ngoma hizo na kuahidi kuwa, watazitumia kuendeleza fani ya ngoma za asili.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu, tulikuwa na shida kubwa ya ngoma za kisasa sasa tumepata. Tutazitumia kukuza sanaa hii ya ngoma za asili” alisema Anna.
Msaada huo wa ngoma za asili aina ya mitoji, umetolewa na BASATA kwa Kundi hilo kufuatia viongozi wake kuwaeleza wadau wa Jukwaa la Sanaa kuwa,wana upungufu wa ngoma tatu za kisasa.
No comments:
Post a Comment