Tuesday, August 17, 2010

VODACOM FOUNDATION KUTUMIA MILIONI 40/-“SHARE & CARE”

Mgeni rasmi Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Issa Shaabani Simba akisoma hotuba yake katika viwanja vya Karimjee leo jioni wakati wa Futari iliyoandaliwa na Kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania kupitia kitengo chake cha Vodacom Foundation maalum kwa watoto yatima wa vituo mbalimbali vya jijini Dar es salaam katika mfungo huu wa mwezi mtukufu wa (Ramadhan) ambapo waislamu kote duniani hufunga kama utekelezaji wa nguzo muhimu katika kumcha mwenyezi mungu.


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii wa Vodacom Foundation umetenga zaidi ya milioni 40/- katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kusaidia watoto wanaolelewa kwenye vituo vya yatima na wale wanaoishi katika shule za bweni.

Msaada huo unaotolewa kupitia kampeni ya ‘Share and Care’ utawalenga watoto kutoka mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam, Tanga, Pemba na Unguja na vifaa kama mchele, unga, mafuta ya kula, madaftari na maharage vitatolewa kama futari kwa watoto hao wanaohitaji upendo hususani katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kufutari iliyoandaliwa na Vodacom Foundation, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Dietlof Mare alisema kwa kutambua umuhimu wa jamii inayofanya nayo biashara kampuni yake imeona irudishe kiasi cha faida wanayoipata kwa wananchi ili kiwasaidie.
Akifafanua alisema kwamba tangu mfuko huo uanzishwe miaka minne iliyopita umeweza kusaidia jamii mbalimbali ya Watanzania ndani ya mfungo wa Ramadhani kwa mara ya tatu sasa hususani katika nyanja za elimu, watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wale wanaosoma katika shule za bweni na kukosa huduma za chakula.
“Kwa mwaka huu kupitia kampeni yetu ya ‘Share and Care’ tutarudisha tulichokipata na tutaweza kuwafikia watoto zaidi ya 3,000 wa mikoa ya Tanga, Pemba, Unguja na kwa kuanzia tayari tumetoa msaada wa takribani milioni 18/- kwa baadhi ya watoto wanaolelewa kwenye vituo vya watoto yatima na kutoka shule za bweni mkoani Dar es Salaam,” alisema Mare.

Naye Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaban Bin Simba ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema mbali ya hafla hiyo kutoa futari isiyozoeleka majumbani pia imetoa fursa kwa waislamu kutoka maeneo mbalimbali kukutana katika kumi la kwanza na kukumbushana juu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha Mufti Simba licha ya kuishukuru kampuni ya Vodacom Tanzania kwa misaada iliyotoa kwa jamii ya waislamu alisema jambo hilo linahitaji pongezi na kutaka liungwe mkono na kuigwa na kampuni zingine nchini.


“Kupitia kampeni hii ya ‘Share and Care’ mliyoianzisha ili kuisaidia jamii ya waislamu katika kipindi hiki cha mfungo natumaini kampuni zingine zitapata fursa ya kujifunza kutoka kwenu,” alisema.

Tofauti na hayo Sheikh mkuu alitoa rai kwa Vodacom Tanzania kuwa kitendo hicho kizidi kuitia moyo kampuni hiyo na kutumia changamoto waliyoipata kurekebisha kwenye mapungufu na kuboresha zaidi katika mafanikio waliyofikia.

No comments:

Post a Comment