Wednesday, August 18, 2010

Miss Vodacom Tanzania kudhaminiwa kwa Bil 1/-
Hapa warembo wakiwasili mjenggoni Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi mtendaji wa Hoteli ya Girraf  Charles Bekoni (kushoto) akiwakaribisha walimbwende kambini hotelini hapo, kulia ni  Afisa Udhamini wa Vodacom, Ibrahim Kaude
Baadhi ya washiriki wakiwa katika ukumbi wa mikutono katika hoteli ya Giraf  kwa ajili ya utambulisho na kukaribishwa kambini hapo.

 Walimbwende wote kwenye picha ya pamoja.


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imesema kuwa, mwaka huu itatumia takribani shilingi Bilioni 1/- ili kufanikisha udhamini wa shindano la Miss Vodacom Tanzania kuanzia ngazi ya awali hadi siku ya fainali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi ya warembo wa Miss Vodacom Tanzania iliyoanza juzi jijini Dar es Salaam, Afisa Udhamini wa Vodacom, Ibrahim Kaude alisema fedha hizo zitatumika kwa kazi mbalimbali ikiwemo usafiri wa warembo ndani na nje, mavazi siku ya fainali na gharama zingine.

Aidha Kaude aliwataka warembo hao kuzingatia maelekezo ya walimu na masharti ya kambi hiyo ili kulifanya shindano la kumtafuta mlimbwende wa mwaka huu kuwa lenye msisimuko kama yalivyo matarajio ya Vodacom Tanzania.

“Hongereni kwa kufikia katika hatua hii, najua safari imekuwa ndefu tangu ngazi ya vitongoji hadi leo katika kambi ya Miss Vodacom Tanzania. Msikate tamaa kwani mwisho wa siku mmoja kati yenu ndiye atakayeibuka kuwa mlimbwende atakayeliwakilisha taifa kwenye medani za kimataifa,” alisema Kaude.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Giraffe Charles Bekoni alisema wamejiandaa kuwapa huduma bora washiriki hao ili waweze kukamilisha matarajio yao ya kuwa warembo wa kimataifa.

“Katika kipindi chote mtakachokuwepo hapa naamini mtafurahia huduma zetu na mtaondoka mkiwa na historia nzuri juu ya hoteli yetu na yote mliyoyapata,” alisema Bekoni.

Naye matroni wa walimbwende hao Gladys Shao alisema kwa jinsi alivyowaona washiriki inaashiria kwamba shindano la mwaka huu halitabiriki na hivyo kuleta ushindani mkubwa miongoni mwa warembo.

“Kwa mwaka jana tetesi zilienea kuwa Miss Vodacom Tanzania anayemaliza muda wake Miriam Gerald angeweza kuwa mshindi na kweli ilitokea. Lakini kutokana na kufanana kwa vigezo na warembo wenye sifa kwa washiriki wa shindano la 2010/11 ni wazi upinzani utakuwa mkali,” alisema Shao.

Warembo 31 walioanza kambi inayofanyika kwenye Hoteli ya Giraffe ni Esther Dennis, Gloria Kaale kutoka kanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shadia Mohamed (Mbeya), Furaha David (Ruvuma), Mary Kagali (Iringa) kanda ya nyanda za juu kusini.

Wengine ni Bahati Chando, Salma Nwakalukwa (Dar City Center) na Consolata Lukosi (Tabata) kanda ya Ilala, Frola Florence, Mary Adam (Morogoro), Angelina Ndege (Lindi) kanda ya Mashariki, Alice Lushiku, Irene Hezron (Dar Indian Ocean) na Amisuu Malik (Sinza) wanaoiwakilisha Kinondoni. Pia wamo Genevieve Emmanuel, Anna Daudi na Britney Urassa (Chang’ombe) kutoka Temeke.

Washiriki kutoka kanda ya Kaskazini ni Glory Mwanga (Arusha), Prinsca Mkonyi (Kilimanjaro) na Jally Murei. Ambapo kutoka kanda ya Chuo Kikuu Huria (OUT) ni Gloria Mosha na Christine Justine.

Kutoka elimu ya juu ni Flora Martin, Pendo Sam (IFM), Rachel Sindbad (UDOM), Fatma Ibrahim (Mara), Buduri Ibrahim, Margareth Godson (Shinyanga) wa kanda ya ziwa na Willemi Etami, Wande Masegese (Dodoma) na Pili Issa wanaoiwakilisha kanda ya Kati.


No comments:

Post a Comment