Sunday, May 15, 2011

OLE WAO WATAKAO CHAKACHUA HALELUYA COLLECTION

MKURUGENZI WA MSAMA PROMOTIONS-  ALEX MSAMA

Na Daniel Mkate
BAADA ya kuenea kwa ‘wachakachuaji’ wa cd’s wa kazi za wasanii mbalimbali nchini, uongozi wa kampuni ya Msama Promotions, umeanza kazi ya kutawanya maafisa wake sehemu mbalimbali nchini kuwasaka wajanja hao wa kazi za wasanii.
Akizungumza na Dira ya Mtanzania juzi, Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama, alisema maafisa wake tayari wameanza kuingia mitaani kuwasaka wanaodurufu kazi za albamu ya Haleluya Collection pamoja na kazi nyingine zilizofanywa na kampuni hiyo.
“Tayari tumeshaanza kuwasambaza maafisa wetu mitaani, kwani wapo wajanja walioanza kudurufu kazi za albamu hiyo iliyotoka hivi karibuni na kuzinduliwa wakati wa tamasha la Pasaka,” alisema Msama.
Msama aliwataka wajanja walioanza ‘kuchakachua’ kazi za albamu hiyo ya Haleluya Colletion, kuacha mara moja kabla ya hawajakamatwa na maafisa hao walioenea Jijini Dar es Salaam kwa sasa.
Alisema kutokana na kazi za Haleluya Collection na albamu nyingine zilizotolewa na kampuni hiyo kuanza kudurufiwa na wajanja, tayari wamepata taarifa toka sehemu mbalimbali kuwa wapo ‘wachakachuaji’ wa albamu hizo na kuziuza mitaani kwa bei poa.
Mkurugenzi huyo wa Msama, alisema albamu halisi ya Haleluya Collection, ina kasha gumu ambalo halipo katika mafuko wa nailoni, tofauti na zile ambazo zinatengenezwa na wajanja wachache hivi sasa.
“Tayari tumetoa namba zetu za 0786 383838 kwa watu mbalimbali ili kufanikisha urahisi wa kuwabamba wajanja hao…pia tutatoa zawadi ya kati ya Sh. Laki 1 hadi Milioni 1 kwa atakayefanikisha kupatikana kwa ‘wachakachuaji’ hao,” alisema Msama.
Aidha, alisema kazi hiyo ya maafisa wa Msama Promotion kuwasaka wachakachuaji hao, itafanyika nchi nzima na hivi wataanza na Jiji la wajanja, Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika mikoa mingine.
Albamu ya Haleluya Collection ilizinduliwa hivi karibuni wakati wa Tamasha la Pasaka lililofanyika katika mikoa ya Dar, Dodoma na Mwanza.

No comments:

Post a Comment