Zanzibar wenyewe wanaita Zenj, ina wasaniii wengi wa muziki wa kizazi kipya wanaokubalika kwa kiwango kikubwa, na wanafanya vyema katika fani hiyo. Miongoni mwa wasanii hao mahiri yumo msanii wa kike aitwaye Jamila Abdallah a.k.a Baby J ambaye amekuwa akifanya vizuri na hata kujinyakulia tuzo lukuki kisiwani humo.
Msanii huyo mwenye urefu wa kiasi, kwa mara ya kwanza alianza kutambulika kwenye anga ya muziki wa bongofleva kwa wimbo wake uliotwa Mapenzi ya Kweli, aliyourekodia ndani ya studio za G Record kwa Omar Saidi Kombo a.k.a KJT, na kweli wimbo huo ulikubalika kwa wapenzi na washabiki wa muziki huo ndani ya Zenj na hata huku bara kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na kufahamika kwa haraka ndani ya gemu, lakini mpaka sasa Baby J hajatoa albamu, anatamba na singo zake tatu ambazo ni Mapenzi ya kweli, aliyomshirikisha msanii Takwa, Moyo wangu umechoka aliyofanya colabo na Pasha, Niache niende aliyomshirikisha Chid Benz. Hivi singo hizi zimekuwa zikimtambulisha vema na kumuweka chat ya juu kabisa kwa wasichana wanaofanya muziki huo kwa upande wa Zanzibar.
"Mpaka sasa sijajua albamu yangu ya kwanza nitaipa jina gani, nasema hivi kwa sababu nyimbo zote nilizotoa naona zote ni kali na zimekubalika, pamoja na hayo yote ndiyo naimalizia malizia ili ikitoka iwe gumzo ndani na nje hata kimasoko pia”, anasema Baby huku akicheka sana.
Baby J ambaye alizaliwa takribani miaka 21 iliyopita ndani ya kisiwa cha karafuu, anabainisha kuwa alianza kujiingiza kwenye fani ya muziki tangu mnamo mwaka 2006, baada ya kufanikiwa kuibuka na wimbo wake wa kwanza uliojulikana kwa jina la Mapenzi ya Kweli.
"Namshukuru mwenyezi Mungu kwa kuweza kunisaidia na kunipa kipaji nilichonacho, kwa kuwa nilipotoa wimbo wangu wa kwanza tu nilibahatika kupata tuzo ya msanii chipukizi wa mwaka wa kike na mwanamuziki bora wa kike wa kizazi kipya kwa mwaka 2008 zilizoitwa Tigo Zanzibar Music Award," anasema Baby J.
Ukiachilia mbali na umri mdogo alionao, Baby J anasema kwa sasa najipanga upya kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi katika fani ya muziki, anasema na kuongeza kuwa pamoja na kupata tuzo kadhaa ikiwemo hii ya mwaka huu 2009 ya kuibuka na tuzo ya msanii bora wa kike, zimenifanya niongeze munkari na juhudi zaidi na kuonesha kuwa hata sisi wanawake tunaweza kufanya vizuri kwa mambo mengi tu.
Baby J anaishukuru familia yake pamoja na walimu wake kwa kumpa sapoti ya kutosha na hata kufanikiwa kwa japo kwa kufanya mambo ambayo nilikuwa nikiota kwa miaka kadhaa iliyopita, mambo ambayo naamini ni makubwa kuliko na umri wangu, na endapo mwenyezi Mungu akinijaalia nitapenda niendelee na masomo ya Uandishi wa Habari," anasema Baby J.
Akibainisha kuhusu mafanikio aliyoyapata, Baby J anasema kuwa mafanikio yapo lakini kwa ukiasi, anasema na kuongeza kuwa mpaka sasa amefanikiwa kunyakua tuzo kwa miaka miwili mfululizo, anasema pamoja na tuzo hizo kwa sasa anachosubiria ni kuhakikisha anaitoa albamu yake na kuipeleke sokoni, na vile vile anatarajia kutoa video yake ya wimbo umpa uitwao Moyo umechoka.
Je Baby J, kwanini anapenda kuimba nyimbo za mapenzi zaidi, anacheka kidogo na kusema kuwa yeye kama msanii yupo katika jamii iliozungukwa na maisha ya mapenzi, anaendelea kusema kuwa kutokana na hali hiyo ndiyo maana kila wakati hukosi kusikia mikwaruzano ya kimapenzi katika jamii fulani, ukiuliza sababu kubwa ni suala la mapenzi, “Yule kajichoma kisu kafa ukiuliza sababu kubwa ni mapenzi, na sasa kila kukicha tunaambiwa kuhusu wakina fataki sasa jamani mimi sitashindwa kujua kinachoendelea, nadhani jibu hapo utakuwa umeshalipata,".analonga Baby J.
Alipoulizwa anazungumziaje suala la ugonjwa wa UKIMWI akiwa kama msanii, anasema kuwa yeye anajitambua vyema na yuko makini katika kupambana na vishawishi vya hapa na pale, “Na pia nipingana na hali ya kuwa na wapenzi wengi wakati hali imekuwa mbaya mpaka inatisha, na nawashauri wasanii wenzangu na jamii kwa ujumla wawe makini katika suala zima la kupambana na ugonjwa huu hatari ambao umekwishapoteza mamilioni ya watu” anamalizia kusema.
No comments:
Post a Comment