Meneja Mzalishaji wa Kundi la Vichekesho la Orijino Komedi, Sekion David ‘Seki’ (aliyesimama) akiongea na wadau wa Jukwaa la Sanaa wiki kwenye Ukumbi wa BASATA.Wengine kutoka kulia ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo, Aristide Kwizela, Msanii Lucas Mhavile ‘Joti’ na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey Mungereza.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey Mungereza akieleza juu ya haja ya wasanii kujitambua na kuthamini kazi zao kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Mdau kutoka Chama Cha Muziki wa Dansi nchini na mshauri wa masuala ya Hakimiliki Francis Kaswahili akishauri masuala mbalimbali kuhusu hakimiliki na shiriki kwenye kazi za Sanaa.
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujitambua kwa kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu katika kazi zao na kutambua thamani yao.
Akizungumza wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika makao makuu ya BASATA, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, Godfrey Mungereza alisema kuwa, kujitambua kwa msanii ni mwanzo wa kuipa kazi yake thamani kubwa kuliko ilivyo sasa ambapo wasanii wamekuwa wakikubali kulipwa malipo kidogo.
“Sanaa ni kazi, sanaa inalipa, ni lazima wasanii wawe na mipango ya muda mfupi na mrefu. Muhimu ni kwa wasanii kutambua thamani yao na kazi wanazozifanya. Ifike mahali wasanii watambue thamani yao ni nini” alieleza Mungereza.
Aliongeza kuwa, kupanda kwa thamani ya msanii kuko mikononi mwa wasanii wenyewe kwa kujitambua na kupanga viwango vya juu katika malipo yao ambayo mtu yeyote atakayewahitaji lazima ayaafiki na ayalipe.
“Ifike mahali msanii au kundi la wasanii walipwe milioni 10 hadi 20 kwa onyesho. Hili linawezekana kwa wasanii wenyewe kutambua thamani ya kazi wanazozifanya na hata kuwa na mipango inayosimamiwa na kutekelezwa kikamilifu” aliongeza.
Awali Meneja Uzalishaji wa Kundi la Orijino Komedi, Sekioni Davidi maarufu kwa jina la Seki akiwasilisha mada kuhusu Sanaa ya Vichekesho na Changamoto Zake alisema kuwa, kundi lake limepata mafanikio kutokana na kutambua thamani ya Sanaa na kupanga viwango vya juu katika malipo yao kwenye maonyesho.
Alisema kuwa, mbali na kupata fedha kutokana na matangazo yanayorushwa kwenye kipindi chao cha Orijino Komedi, wamekuwa wakipata fedha nyingi kupitia maonyesho ambayo kwa mujibu wake wamekuwa wakiweka viwango vikubwa kwa wanaowahitaji kwenye maonyesho.
“Yeyote anayelihitaji kundi kwenye onyesho lazima achukulie sanaa yetu kama kazi. Hatutaki mtu anayeichukulia sanaa kama zamani, tunataka mialiko michache lakini yenye thamani kubwa kwetu” aliongeza Seki.
Kwa upande wake Msanii Lucas Mhavile maarufu kwa jina la Joti alisema kuwa, wanatumia muda mwingi kujituma kwenye kazi za Sanaa ili kunufaika na si vinginevyo hivyo, viwango na thamani yao lazima iwe juu.
No comments:
Post a Comment