Tuesday, October 11, 2011

BASATA: JUKWAA LA SANAA NI DARASA KWA WASANII

Mmoja wa Wanakamati wa Kamati ya Tunzo za Muziki wa Injili, Haris Kapiga (Kushoto) akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA kuhusu Changamoto katika kuuvusha mipaka muziki wa Injili. Kulia ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo, Aristide Kwizela.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari Bw. Godfrey Lebejo (Kushoto) akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa. Aliwataka wasanii kulitumia Jukwaa hilo kama darasa la kukuza uelewa na stadi zao.
Msanii wa Muziki wa Injili aliyejitambulisha kwa jina la Syllivanus akichangia mawazo kwenye Jukwaa la Sanaa.
Sehemu ya wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala kwa makini

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kuwa, programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila wiki makao makuu ya baraza hilo ni elimu tosha kwa wasanii kwani mada zinazogusa maeneo mbalimbali kwa wasanii zimekuwa zikiwasilishwa.
Akizungumza wiki hii kwenye programu hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Bw. Godfrey Lebejo alisema kuwa, Baraza limekuwa likialika wataalam katika fani mbalimbali kwa malengo ya kuwakutanisha na wasanii na kuwapa stadi ambazo huwasaidia katika kuendeleza vipaji na kazi zao.
“Jukwaa hili limekuwa ni sehemu ya kuibua mijadala na mawazo kwa ajili ya kusongesha mbele gurudumu la Sanaa. Ni darasa la stadi ambalo kwa mtu yeyote anayetaka kukuza taaluma na kipaji chake anaweza kulitumia” alisema Lebejo.
Aliongeza kuwa, mada ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na wataalam kutoka fani mbalimbali ni hazina tosha kwa wasanii na wadau wengine wa elimu ambao wangependa kufanya stadi zao katika tasnia hii ya Sanaa.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Changamoto Katika Kuuvusha Mipaka Muziki wa Injili mmoja wa wanakamati wa Tuzo za Muziki wa Injili nchini, Haris Kapiga alisema kuwa, kuna kila sababu ya wasanii wa muziki wa injili nchini kufanya kazi zao kitaalam zaidi na kutumia teknolojia ya mawasiliano katika kujitangaza.
“Ni ajabu sana, kuna wasanii wengi wa muziki wa injili ni maarufu sana lakini hawapatikani kwenye mitandao kama ya Facebook, twitter na mingineyo ambayo hutumiwa na wasanii wengi katika kujitangaza” alieleza Kapiga.
Aliongeza kuwa, hali hiyo ni tofauti na wasanii wa nje kama Rebecca Malope ambao ukiingia kwenye mitandao ya mawasiliano ni rahisi sana kupata taarifa na hata kazi zao hivyo kutanua fursa zao za kujitangaza na kujipatia kipato.
Kuhusu utafiti alioufanya kwa kuzungukia maduka mbalimbali ya usambazaji kazi za Wasanii wa muziki wa Injili Bw. Kapiga alisema kuwa, wasanii kutoka nje kama wale wa Kundi la Ambassadors of Christ kutoka Rwanda na Sara K wa Kenya wamekuwa wakifanya vizuri na kuwazidi wasanii wa ndani.
Alitoa wito kwa wasanii kutumia fursa mbalimbali kujitangaza hasa kutumia teknolojia za kisasa na kutengeza kazi zenye ubora ili kazi zao ziweze kuvuka mipaka na kufanya vizuri zaidi.


No comments:

Post a Comment