b..

B1

Wynem

animation

Tuesday, October 5, 2010

WASANII WATAKIWA KUTUNZA KUMBUKUMBU YA KAZI ZAO.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa,Dkt Paul Msemwa
 
Umati wa wadau ukifuatilia kwa makini mada kwenye Jukwaa la Sanaa.
Mzee Nkwama Bhalanga ambaye ni Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi yeye alitaka Zijengwe hifadhi za Sanaa na Utamaduni katika ngazi mbalimbali nchini kuanzia wilayani.
Wasanii wa Muziki Kizazi kipya wakifurahia jambo baada ya kuahirishwa kwa Jukwaa la Sanaa.Kutoka Kulia ni Dar Shopper,Mzee Nkwama Bhalanga,Mtoto wa Kitaa,Gheto King na Yuda Skills.

Wasanii wametakiwa kutunza kumbukumbu ya kazi zote wanazozifanya ikiwa ni pamoja na kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za kazi za sanaa za kale ili kuchota ujuzi wa kale na kuboresha sanaa wanazozifanya.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa,Dkt Paul Msemwa wakati akiwasilisha mada yake kuhusu ‘Uhifadhi wa Sanaa za Asili na Changamoto Zake’ kwenye Jukwaa la Sanaa, linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kukutanisha wadau wengi wa sanaa.
Alisema kwamba uhifadhi wa kazi za sanaa ni muhimu sana kwani ndiyo chanzo kikubwa cha kujua ni kwa kiwango gani sanaa imebadilika na ni kwa jinsi gani wasanii wataweza kutumia kazi za kale za sanaa katika kuboresha zile wanazozizalisha sasa.
Aliongeza kwamba, sanaa haiwezi kukua kama wasanii watakuwa ni wa kujifungia ndani ya boksi na kubuni vitu vyao bila kutaka kutafiti na kujifunza sanaa za kale zilivyokuwa ili nao waweze kuboresha na kuongeza vionjo kulingana na nyakati tulizonazo sana.

“Ukuzaji wa Sanaa huanza na kujua wengine wanafanya nini halafu ukishajua sasa unaweza kuongeza vionjo na ubunifu kulingana na nyakati zilizopo lakini pia uhitaji wa soko la kazi za sanaa” Alisisitiza Dkt.Msemwa.
Aliyataja matatizo ambayo yanasababishwa na wasanii kutokutunza kumbukumbu ya kazi zao kuwa ni pamoja na kazi zao kutokuthaminiwa,kuuzwa kwa bei za chini,kuibiwa hakimiliki, kuharibiwa, kutoroshwa nje ya nchi pasi na mtu kujali na wasanii kushindwa kujua tarehe na muda kazi zao ziliozalishwa.
Sakata la wasanii hususan wa muziki kupuuzia kutunza kumbukumbu ya kazi zao liliibuka Kwenye Jukwa la Sanaa mwezi mmoja uliopita wakati Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe akiwasilisha mada yake Kuhusu ‘Mwelekeo wa Tunzo za Muziki Tanzania na Changamoto Zake’ ambapo alisema kwamba, wasanii wamekuwa hawatunzi kumbukumbu za kazi zao hali ambayo imekuwa ni changamoto katika uingizaji wa nyimbo zao kwenye tunzo za Muziki Tanzania (Kilimanjaro Music Awards).
Mbali na kuwashauri wasanii kujenga utamaduni wa kuhifadhi kazi zao, aliwashauri kutembela hifadhi za sanaa za kale na kazi zingine za utamaduni ili kujijenga kisanii na kupata kujifunza sanaa za kale zilivyokuwa zinaendeshwa ili sasa waweze kupata pa kuanzia.
Kwa uapande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba, utunzaji wa kazi za sanaa ni muhimu sana kwani ndiyo njia pekee ya kuirithisha sanaa kwa vizazi vijavyo.Aliongeza kwamba, lazima kuwepo na utaratibu wa wasanii kuhifadhi kazi zao ili kuhakikisha hazipotei na kusahaulika.
Wadau wengi waliochangia kwenye Jukwa la Sanaa waliishauri serikali kuanzisha Hifadhi za Kazi za Sanaa na Utamaduni katika ngazi mbalimbali za wilaya na mikoa badala ya ilivyo sasa ambapo hupatikana katika maeneo machache.Walisema kwamba, maafisa utamaduni wapewe kazi ya kuratibu zoezi hili ili kufufua utamaduni.
Jukwaa la Sanaa litaendelea tena wiki ijayo na wadau wa sanaa kama kawaida watakuwepo kujadili masuala mbalimbali yahusuyo tasnia hii.

No comments:

Post a Comment