Tuesday, April 24, 2012

WASANII WA BONGOFLEVA WAPEWA DARASA

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha muziki wa asili nchini, Che Mundugwao akiongea na wadau wa Jukwaa la Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha mada iliyohusu Utunzi na Ubora Katika Tungo za Muziki. Kulia ni Maafisa kutoka BASATA, Aristide Kwizela na Agnes Kimwaga.
Mkongwe wa Muziki wa dansi nchini, Mzee Kassim Mapili akichukua notisi ya kile kinachojadiliwa kwenye Jukwaa la Sanaa. Aliwaasa Wasanii kujifunza na utumizi wa ala katika muziki.
Mdau wakichangia mjadala kwa hisia

Na Mwandishi Wetu
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wameshauriwa kuwa na msimamo katika aina ya mahadhi ya muziki wanaoimba kuliko ilivyo sasa ambapo wengi wamekuwa wakichanganya na kushindwa kueleweka.
Wito huo umetolewa wiki hii na wadau wa Sanaa wakati wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo walisema kuwa, halil hiyo imeufanya muziki wetu ukose utambulisho na kushindwa kufanya vizuri kimataifa. “Wasanii wetu wamekuwa wakichanganganya mahadhi (aina) ya muziki wanaoimba.Leo anaimba reggae, kesho zouk mara muziki wa asili, hii inamfanya msanii asieleweke aina ya muziki anaoimba lakini pia tunakosa ubobezi kwenye aina hizi” alisema Che Mundugwao ambaye ni makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki nchini.
Aliongeza kuwa, kubadilika-badilika kwa wasanii kwenye aina ya muziki wanaoufanya si tu kumeufanya muziki wetu ushindwe kuvuma kimataifa bali pia unakosa utambulisho kwenye aina zingine za miziki zinazopatikana na kufahamika duniani kote.
“Muziki ni lugha ya Dunia, aina zake zinafahamika duniani kote.Tunachopaswa kufanya ni kutumia vionjo vya asili yetu ili kuleta utofauti. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwatumbuiza watanzaia wenzetu waishio ughaibuni tu na si kufanya matamasha ya kimataifa” alisistiza Che Mundugwao ambaye pia ni msanii wa muziki wa asili.
Mdau mwingine aliyefahamika kwa jina la Mbile Hango alionya kuwa, wasanii wetu wataendelea kuvuma kwa muda mfupi na kutoweka kama hawatazingatia taaluma na ubobezi katika aina fulani ya muziki.
Aliongeza kuwa, ni vigumu kwa wasanii kuimba kwa kunakiri muziki kutoka nchi za nje kama ile ya qwaito yenye asili ya Afrika Kusini halafu wategemee kupata fursa ya kuuza kazi zao nje na kushiriki matamasha ya kimataifa.
“Ukinakiri muziki kutoka nje maana yake huna kipya cha kupeleka nje, tutaendelea kuvuma humu humu ndani” alionya.
Mjadala wa wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa ulijikita kwenye Ubora katika Utunzi wa Tungo za Muziki

No comments:

Post a Comment