Tuesday, April 24, 2012

SHINDANO LA KUIBUA VIPAJI LA KILI, LILIVYOKUWA DODOMA

majaji Kazini, hapa wakisikiliza muongozo kutoka kwa muendesha zoezi, Irene Kiwia, ambaye hayupo pichani, kutoka kushoto ni henry Mdimu, Joseph Haule, Queen Darleen, na Juma Nature
Mmoja wa washiriki Juma Madaraka akionesha ujuzi wake wa kuimba na kucharaza gitaa mbele ya majaji
Hawa ndio 20 bora waliokuwa wameingia katika fainali za mashindano hayo kutoka mkoani Dodoma
Washiriki wakipongezana baada ya tatu bora itakayowakilisha mkoa wa Dodoma kutajwa
Tatu bora, kutoka kushoto ni halima ramadhani, katikati ni Juma Madaraka na mwisho kabisa ni Issa Dubat
Washiriki wakifurahi pamoja baada ya washindi kutajwa

Na Mwandishi wetu
Baada ya siku mbili za usaili wa jumla ya washiriki 247 waliowania nafasi ya kupanda jukwaa moja na washindi wa tunzo za Kili wa mwaka 2012, hatimaye wawakilishi wa mkoa wa Dodoma wamepatikana jana mchana katika zoezi lililoonekana kuwa gumu kutokana na washiriki hao kuwa na vipaji vya hali ya juu vinavyofanana.
Katika zoezi hilo lililofanyika katika ukumbi wa Club maarufu mkoani humo inayojulikana kwa jina la 84, kati ya wasanii 247, ni wasanii watano tu wenye jinsia ya kike ndio walijitokeza kushiriki.
Kazi ya mchujo kwa wasanii hawa ilifanyika kwa takriban masaa 29 ambapo majaji wanne waliifanya, wakiongozwa na msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule, na mwanamuziki mwingine maarufu wa muziki huo Juma Kassim Nature, mshindi wa tunzo ya wimbo bora wa ragga kwa msimu huu Queen darleen na Mhariri wa Burudani wa Magazeti ya Mwananchi Communications.
Katika mchujo wa kwanza, jumla ya wasanii 200 waliondolewa katika mashindano, kisha wakabakia 47 ambao nao walipopita mbele ya majaji kwa mara ya pili, walijikuta wakiondoka 27 na kubakia 20 ambao waliingia katika fainali ya awali iliyofanyika siku iliyofuata.
Fainali nayo ilienda kwa michujo miwili ambapo katika mchujo wa kwanza, wasanii watano tu walibakia na mchuko wa pili ulipopita, wakabakia watatu ambao Jumamosi hii watakuwa ni wasanii wa awali kupanda katika jukwaa la tamasha kubwa la washindi wa tunzo za Kili mwaka huu ambapo kati yao, atakayeimba vizuri atadhaminiwa na bia ya Kilimanjaro kuendeleza muziki wake na huyo pia atakuja kwenye tamasha kubwa la washindi litakalofanyika jijini Dar es salaam.
Akitangaza washindi, mmoja kati ya majaji walioonekana kuwa chachu ya mchuano huo henry Mdimu, aliwataja Halima Ramadhani, Juma madaraka na Issa Dulat kuwa ndio waliofanikiwa kufikia vigezo vya kuwa wasanii bora kabisa kutoka mkoani Dodoma kwa mwaka huu ingawa dhahiri vipaji vilionekana kuwa vingi kuliko walivyotegemea.
"Haikuwa kazi rafisi, ilikuwa inatupa wakati mgumu na kama sio maelekezo ya waandaaji huenda tungejikuta tu8nachukua hata watano baada ya watatu", alisema Jaji huyo baada ya shughuli kuisha.
Wiki hii mpambano utaendelea katika mkoa wa mwanza, ambapo Jumamosi, wasanii wa mkoa wa Mwanza watakuwa wakiisaka nafasi hiyo katika ukumbi wa Villa Park.

No comments:

Post a Comment