PRESS RELEASE
MASIKITIKIO JUU YA KIFO CHA MSANII STEVEN CHARLES
KANUMBA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi
makubwa taarifa ya kifo cha Msanii wa filamu Steven Charles Kanumba
kilichotokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi ya Tarehe 07/04/2012 baada ya
kuanguka ghafla akiwa nyumbani kwake Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa
maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa
kihistoria. Kufiwa na msanii huyu mahili
kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na Taifa kwa
ujumla kutokana na ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa yetu nje
ya mipaka.
Kanumba atakumbukwa kwa moyo wake wa kujituma na kuthamini kazi ya Sanaa
toka akiwa Kundi la Maigizo la Kaole ambapo moyo wake huo ulimfanya awe miongoni
mwa wasanii walioleta mageuzi kwenye tasnia ya filamu kwa kuifanya kuanza
kupendwa na wadau wengi zaidi.
Aidha, atakumbukwa kwa juhudi zake za kuinua vipaji vichanga katika tasnia
ya filamu ambapo mara kadhaa katika kazi alizoziandaa alishirikisha wasanii
wachanga ambao BASATA inaamini watakuja kuwa hazina kubwa kwa taifa letu.
BASATA linatoa pole kwa familia ya marehemu na Wasanii wote katika kipindi
hiki kigumu. Ni vema wasanii wote tukatumia kipindi hiki kutathimini kwa pamoja
michango yetu katika kukuza sekta ya Sanaa ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja
wetu lakini pia tukiyaenzi yale yote mema yaliyofanywa na Steven Charles
Kanumba.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba mahali pema peponi.
AMEN
Sanaa ni Kazi Kwa
Pamoja Tuikuze na Kuithamini.
Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment