Thursday, April 12, 2012

CECAFA YATUMA RAMBI RAMBI MALAWI

Rais Bingu wa Mutharika - Enzi ya uhai wake
BARAZA la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetuma salamu za rambi rambi kwa Shirikisho la Soka Nchini Malawi (FAM) baada ya rais wa nchini hiyo Dr Bingu wa Mutharika kufariki dunia. 
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye katika taarifa aliyoitoa alisema wamehuzunishwa na kifo hicho kilichotokea Alhamisi iliyopita kutokana na ugonjwa wa moyo kwenye Ikulu mpya ya Malawi iliyopo Mjini Lilongwe.
"Tunaomboleza na nyinyi na watu wa Malawi msiba huu mkubwa, ambapo tumepoteza mtu muhimu mwenye rekodi nzuri ya kuchapa kazi,"alisema Musonye.
Alisema,"tunasali ili watu wa Malawi ambao wapo pamoja na Cecafa wauchkue msiba huu kwa ustahimilivu mkubwa na waweze kupata rais mwingine kwa amani."
Pia alisema,"taarifa hii yangu ya maombolezo naomba imfikie mke wa rais, watoto wake, watu wa karibu wa familia na watu wa Malawi kwa ujumla."
Mwili wa Mutharika upo nchini Afrika Kusini na unatarajiwa kusafirishwa mpaka nchini Malawi kwa ajili ya mazishi Aprili 23 kwenye shamba lake huko Ndata Kusini mwa mji wa Thyolo.
Malawi ilikuwa mwanachama wa kamili wa Cecafa tangu mwaka 1970, lakini katika miaka ya 90 ilijiunga na Baraza la Vyama vya Soka vya Kusini mwa Afrika Cosafa.

No comments:

Post a Comment