Thursday, January 26, 2012

PINDA: SIFIKIRII KUGOMBEA URAISI 2015

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ikulu, Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman


Ramadhan Semtawa
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezungumzia mambo muhimu kumi na moja yanayogusa nchi kwa sasa yakiwemo ya kiuchumi na kisiasa huku akiwashangaa wanaotumia nguvu nyingi kuwania nafasi ya urais akisema hawajui mzigo mkubwa wa kuongoza taasisi hiyo.Katika mkutano wake na wahariri na wawakilishi wao uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam jana, Pinda alisema: “Kwa dhati sifikirii kugombea nafasi hiyo ya juu kwani ni mzigo mkubwa.”Alisema kuna watu wanautaka urais kwa nguvu na kuhoji kama wanajua mzigo mkubwa uliopo katika taasisi hiyo au wanafurahia mazingira yake ili wakanufaike kiuchumi na kibiashara.“Kuna watu wanautaka kweli urais... wanautaka kwelikweli, lakini kuutaka na kuupata ni vitu tofauti. Sijui kama wanautaka ili wawatumikie Watanzania au kwa sababu tu ya mazingira mazuri yaliyopo pale ili waweze kufanya biashara au wanufaike kiuchumi.”Alisema mtu anayejua mzigo mkubwa uliopo Ikulu kamwe hawezi kuutaka kama baadhi wanavyofanya: “Wakati mwingine huwa nikienda Ikulu namwambia ndugu yangu Rais pole. Ikulu ni mzigo mkubwa.”
“Sasa hawa wanaoutaka kwa nguvu, ni kweli wanataka kwenda kubeba mzigo huo mzito ? Mimi siko tayari. Sasa wanaoutaka urais kwa nguvu labda wawe wanakwenda pale kufurahia mazingira ya Ikulu kama kufanya biashara lakini si kutumikia Watanzania.”Alisema Watanzania wanahitaji Rais ambaye atawatumikia kwa dhati na anayejua matatizo yao na huyo ndiye ambaye wenyewe watamchagua mwaka 2015 wakati wa uchaguzi.Alisema anajivunia muda mwingi alioutumikia umma tangu Ikulu na hadi nafasi ya Waziri Mkuu na kuongeza: "Sasa hivi ni Waziri Mkuu. Hapa ni shule tosha najivunia kutumikia umma hadi hapa nilipo. Panatosha nasema hili kwa dhati.”Wakuu wa Wilaya Waziri Mkuu alikiri kuwepo wilaya ambazo zinakaimiwa na wakuu wa wilaya na kuongeza kwamba mchakato wa kukamilisha uteuzi wao umeshakamilika na kinachosubiriwa ni kutangazwa na Rais.Alisema kuchelewa kukamilika kwa mchakato huo kulitokana na matatizo ya kisheria katika baadhi ya maeneo, kwani kulikuwa na mchakato wa kupokea maoni ya wapi kuwe makao makuu lakini, hilo na mengine yamekamilika na anayesubiriwa sasa ni mkuu huyo wa nchi.KatibaAkizungumzia mchakato wa Katiba, Pinda alisema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha nchi inapata Katiba bora ambayo itagusa maslahi ya makundi tofauti ya kijamii.Alisema hivi sasa imeundwa timu ndogo ya wataalamu ambayo itaangalia namna ya kufanya maandalizi ya kufanikisha utendaji kazi wa tume ya kuratibu mchakato huo punde itakapoundwa.Alifafanua kwamba timu hiyo haina uhusiano wala haitafanya chochote kuhusu mapendekezo ya uteuzi wala kuingilia mchakato wa kisheria wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, bali itaangalia namna ofisi ya tume itakavyopatikana, maslahi kama mishahara, vitendea kazi, magari na miundombinu ya mawasiliano katika utendaji.Pinda alisema timu hiyo ambayo imeundwa na Katibu Mkuu Kiongozi, itafanya kazi hiyo kwa umakini ili kuhakikisha tume itakapoundwa na kuanza kazi, maandalizi yote ya msingi yanakuwa yamekamilika.Kuhusu mapendekezo ambayo Rais amekuwa akiyapokea katika kipindi hiki ambacho tayari sheria imekwishapitishwa na Bunge, alisema anasubiri maelekezo kutoka kwa mkuu huyo wa nchi kuona kama kuna mapendekezo ambayo yanaweza kupelekwa bungeni na sheria hiyo kufanyiwa marekebisho madogo ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya wadau wote.Alisema dhamira ya Serikali na Rais ni kuhakikisha kwamba Katiba inayopatikana inakuwa yenye matakwa ya pande zote husika, huku akitoa mfano kwamba kama Chadema inataka Serikali tatu za katika muundo wa muungano hilo litajulikana katika kura za maoni na kama CCM wanataka Serikali mbili pia litajulikana katika kura za maoni.Posho za wabungeAkizungumzia posho za wabunge, Pinda alisema tatizo kubwa lilijitokeza tangu mwanzo ni ukosefu wa taarifa sahihi kwa umma hali iliyoibua mjadala na mgongano wa lugha kati ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashillilah.Alisema wakati mjadala ulivyoibuka, ni kweli Spika alimwandikia barua Rais kuomba nyongeza hiyo ya posho lakini mkuu huyo wa nchi alikuwa bado hajaidhinisha posho hizo.“Kwa hiyo, kwa lugha rahisi ingekuwa ni kusema hivi... ni kweli tumeomba nyongeza ya posho kwa mheshimiwa Rais lakini hadi sasa hajaidhinisha, atakapoidhinisha au vinginevyo tutasema. Lakini, ikatokea huyu anasema hivi na yule hivi.”Hata hivyo, alisema tayari Rais Kikwete amekwisharejesha suala hilo kwake (Pinda) ili kuendelea na taratibu nyingine zaidi ambazo atatoa maelekezo bungeni kuona namna ya kulimaliza suala hilo bila mvutano.Pinda alisema ingawa kumekuwa na malalamiko, lakini wabunge wana matatizo ya msingi ambayo yanatokana na makato makubwa ya mikopo, kusaidia wapiga kura majimboni na mengine mengi.Alisema serikalini kiwango cha posho ya vikao kwa siku kwa watumishi wa ngazi za juu ni Sh200,000 kwa ngazi ya kati Sh150,000 na nyingine Sh100,000 na kuongeza: “Hivyo, siyo vibaya sana na hata wabunge wakiongezewa. Ni jambo linaloweza kueleweka kama watu watalizungumza jambo hili kwa utulivu.”Pinda alisema tofauti na viongozi wa Serikali kama yeye, wabunge wanajigharamia wenyewe nyumba, magari, mafuta, matengenezo na huduma nyingine za kuwasaidia wananchi, hivyo akataka jambo hilo lizungumzwe bila jazba.UchumiAkizungumzia mwenendo wa uchumi, alikiri kwamba mfumuko wa bei ni tatizo kubwa linalotikisa nchini lakini, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inafanya kila jitihada kuhakikisha unashuka.Alisema mfumuko huo umechangiwa na matatizo ya uchumi wa dunia ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta ambayo kwa sasa pipa moja ni Dola 100 za Marekani katika soko la dunia na matatizo ya mgawo wa umeme.Alisema kipindi cha Julai mwaka jana, mfumuko ulikuwa asilimia 13, Septemba asilimia 16.8, na kushuka kidogo hadi 12.7 ikilinganishwa na asilimia 5.5 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2010.Hata hivyo, alisema mwelekeo wa ukuaji wa uchumi si mbaya kwani lengo kwa mwaka 2011 ilikuwa ni ukuaji wa asilimia sita, lakini robo ya kwanza ya mwaka huo uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.8, ya pili asilimia 6.7 na robo ya tatu iliyoishia Septemba ilikuwa kwa asilimia 6.3, hivyo kuonyesha uchumi mpana wa taifa bado uko imara.Alisema katika kipindi hicho, sekta ya ujenzi ilichangia kwa asilimia 13.2 mawasiliano asilimia 12.9, sekta ya fedha asilimia 11.3 na sekta ya biashara ilichangia kwa asilimia saba.  Kuhusu chakula, alisema ingawa baadhi ya mikoa kama Arusha na Kilimanjaro mazao kama mahindi yameathiriwa na ukame, bado uwezo wa  nchi kujitosheleza kwa chakula kuelekea kipindi cha  Januari hadi Februari bado upo kwani maeneo ya kanda ya ziwa yanatarajiwa kuzalisha mazao ya kutosha.Akizungumzia mpango wa dharura wa umeme uliopitishwa na Bunge alisema unaendelea vizuri ingawa hadi sasa zimepatikana megawati 270 kati ya 300 zilizokuwa zimekusudiwa, ambazo ni sawa na asilimia 90.Katika Bunge la Bajeti la mwaka jana, Serikali iliomba Sh1.2 trilioni za mpango huo wa dharura wa kukabiliana na mgawo wa umeme, ambazo zingeanza kuzalisha umeme kuanzia Agosti hadi Desemba, kwa awamu ya kwanza.JairoKuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge katika sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema kwa sasa hatua za Serikali ziko Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili atoe mapendekezo yake ya kitaalamu.

No comments:

Post a Comment