Tuesday, January 25, 2011

BASATA: WASANII PIMENI UKIMWI MTAMBUE AFYA ZENU.Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA, Godfrey Lebejo Mngereza akieleza juu ya haja ya wasanii kupima afya zao.
 Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Parapanda Mgunga Mwamnyenyelwa akionesha moja ya kazi zinazotazamiwa kufanywa na kundi lake hivi karibuni.
  
Mratibu wa Tamasha maarufu la Sauti za Busara linalotazamiwa kuanza Februari 9 mwaka huu Kwame Mchauru akichangia maoni kwenye Jukwaa la Sanaa.
Muelimishaji rika kutoka Shirika la AMREF, Bw. Bahati Mitula akitoa elimu kwa wasanii dhidi ya UKIMWI kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA. Baada ya elimu jumla ya wadau 107 wa Jukwaa la Sanaa walipata fursa ya kupima kwa hiari afya zao.Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii na wadau wa sanaa kwa ujumla kujenga utaratibu wa kupima UKIMWI  mara kwa mara ili kutambua afya zao na baadaye kuweza kupanga mipango yao ya maisha na shughuli zao za sanaa.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mwenyekiti Jukwaa la Sanaa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA George Lebejo Mngereza wakati wa zoezi maalum la kupima UKIMWI kwa hiari lililoendeshwa na program ya Jukwaa la Sanaa kwa kushirikiana na Shirika la AMREF kupitia mradi wa Angaza.
“Wasanii wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu wengine kupima UKIMWI huku wao wenyewe wakibaki nyuma wakati wako katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa,nadhani sasa wanapaswa nao kuwa mstari wa mbele katika kutambua afya zao ili sasa waweze kupanga mikakati katika shughuli zao za sanaa na maisha yao kwa ujumla” alisema Mngereza.
Aliongeza kwamba BASATA imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za mafunzo dhidi ya UKIMWI kwa wasanii ambayo yamekuwa yakiambatana na zoezi la upimaji kwa hiari na lengo kuu la zoezi hilo ni kuwapa fursa wasanii ambao wamekuwa wakitumiwa kama daraja la kuhamasisha watu mbalimbali nao kufahamu kwa kina gonjwa hili na kujua jinsi ya kuliepuka lakini pia kutambua afya zao ili kuishi kwa tahadhari.
“Sote tutakumbuka kwamba Oktoba 25 mwaka jana BASATA iliendesha zoezi kama hili la elimu dhidi ya UKIMWI kwa wasanii na upimaji. Hii ni fursa nyingine kwa wasanii na wadau wa sanaa kwa ujumla kufanya hivyo ili kutambua afya zao” alisisitiza Mngereza.
Katika zoezi hilo ,jumla ya wadau 187 walihudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa ambapo kati yao  107 walipata fursa ya kupima kwa hiari na hakuna hata mmoja aliyekutwa ameathirika.Idadi hii ni ni zaidi ya wale wa zoezi lililopita kwani 79 tu ndiyo walipima.
Awali kabla ya zoezi la kupima, Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Parapanda Mgunga Mwamnyenyelwa aliwasilisha mada kuhusu Jinsi ya Kuifanya Sanaa na Utamaduni Wetu kutambulika kimataifa ambapo alisisitiza umuhimu wa wasanii wa muziki kuzingatia fani na maudhui ili kuweza kuzifanya kazi zao kuvuka kimataifa.
Aidha,alitumia fursa hiyo kutangaza tamasha kubwa la tamthiliya linalotazamiwa kuanza Januari 28 na kumaliza Januari 29, 2011 kwenye Ukumbi wa Utamaduni wa Ubalozi wa Urusi ambapo litahusisha wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari na baadaye wadau wengine.

No comments:

Post a Comment