Wednesday, February 16, 2011

WAANDAAJI MUZIKI WAILILIA BONGO FLEVA


Kulia ni Muandaaji chipukizi wa muziki wa kizazi kipya anayekuja kwa kasi nchini kutoka Studio za FishCrab,Lamar akiweka msisitizo kwenye mada iliyowasilishwa kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA. Pembeni yake ni Mtaalam wa Muziki John Ndumbaro kutoka mkoani Morogoro.
Muandaaji wa Muziki kutoka Studio za MJ, Joachim Kimario ‘Master J’ (Kulia) akichangia mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa, BASATA.Kulia kwake ni muandaaji mwenzake Allan Mapigo.

Na Mwandishi Wetu
Waandaaji mahiri wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini Joachim Kimario (Master J), Lamar na Allan Mapigo wamedai kwamba,muziki wa kizazi kipya maarufu kwa jina la Bongo Flava umepoteza muelekeo na juhudi za makusudi zinahitajika katika kuurudisha kwenye mstari na kuupa utambulisho wa kitanzania.
Wakizungumza katika mjadala mkali kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa, waandaaji hao wa muziki walitupa lawama kwa watangazaji wa vituo vya redio na TV kwamba ndiyo chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa muziki huo kwa kile walichoeleza kwamba, hakuna utaratibu wa kuchuja nyimbo kabla ya kwenda hewani na baadhi hawana utaalam wa kazi zao.
Aidha, waliongeza kwamba pamoja na wao kujitahidi kuandaa midundo kwa kufyonza kutoka jamii za kitanzania, wasanii wa hapa nyumbani wamekuwa ni wa kuiga kila kitu wanapoingia studio na hawako tayari kubadilika wanapoelekezwa hali ambayo imeufanya muziki uhame kutoka kuwa wa jamii ya Tanzania na kuwa ule wenye kunakiri kila kitu kutoka nje hususan Marekani.
“Kwa sasa wasanii wanachokifanya ni kusikiliza muziki wa nje na kuja kuingiza kwenye muziki wao.Wamekuwa wakikopi kila kile msanii wa nje anachofanya kuanzia kuvaa na kuimba, wanataka wafanane na Jay Z hata wakija studio wanataka watengenezewe sound (midundo) kama ile ya nje” alisema Lamar kutoka Studio za FishCrab.
Kwa upande wake Master J ambaye ni mmiliki wa Studio za MJ alisema kwamba,siku hizi wanamuziki hawaangalii mazingira ya jamii za kitanzania tofauti na zamani, wamekuwa ni wa kuimba mambo yasiyofaa na yasiyopatikana katika jamii yetu bali ile ya Marekani hali ambayo imezidi kuutokomeza muziki wa kizazi kipya.
“Zamani tulikuwa na Hip Hop kama za akina 2 Proud ambaye kwa sasa anajiita Mr.Two (Sugu).Walikuwa wanaimba Hip Hop yenye kubeba matatizo halisi ya jamii ya Tanzania , Sugu aliimba nyimbo kama mikononi mwa polisi, miaka chini ya 18 na zote mbali ya kugusa matatizo yaliyopo ya jamii zilipendwa na kufanya vizuri tofauti na sasa” alisisitiza Master J
Aliongeza “Ujio wa redio na televisheni zisizozingatia utaalamu (professionalism) kwa watangazaji wake bali swaga (ujanja ujanja) na vipaji tu vya kuongea ni moja ya sababu ya kupoteza dira kwa muziki na hapo ndipo mambo yalianza kuharibika”.
Katika Jukwaa hilo la Sanaa pamoja na waandaaji wa muziki hao kutoa michango yao kuhusu mwenendo wa muziki wa kizazi kipya nchini, Mtaalam wa muziki John Ndumbaro alitoa maelezo ya kina kuhusu sekta hiyo ya sanaa ambapo mada ilikuwa ni Changamoto Katika Kutengeneza Muziki wenye Utambulisho wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment