Saturday, February 19, 2011

Tamasha la Pasaka kusaidia wahanga wa mabomu Gongo la Mboto


 
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka la
nyimbo za Injili, Alex Msama (kulia) akimkabidhi mtangazaji wa Radio Clouds, Anthonio Nugazi, magunia yenye vyakula
mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 3 ikiwa ni msaada kwa ajili ya walioathirika kwa mabomu ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Hafla hiyo ilifanyika Makao Makuu ya Clouds,
Mikocheni, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka la
nyimbo za Injili, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa
habari baada ya kukabidhi msaada wenye thamani ya sh. milioni 3 kwa waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam jana.

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Msama Promotions ambao ndio wanadaaji wa Tamasha kubwa la Pasaka, Alex Msama amesema kwamba kiasi cha fedha zikazopatikana katika tamasha hilo, zitatumika kuwasaidia waathirika(wahanga) wa mabomu yaliyotokea kwenye kambi ya jeshi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Msama amesema hayo baada ya kuwakabidhi waathirika wa milipoko hiyo msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya ya shilingi mil 3.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ndiye aliyekabidhi msaada huo leo katika ofisi ya redio ya Clouds FM iliyoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Vitu vilivyotolewa ni magunia manne ya mchele, kila moja likiwa na kilo 120, magunia mawili ya maharage, magunia 10 ya unga wa mahindi, mifuko miwili ya sukari, mifuko mitatu ya unga wa ngano yenye kilo 25 kila moja na ndoo mbili za mafuta ya kupikia.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Msama alisema wameguswa na waathirika hao, na pia wanafanya hivyo ikiwa ni kutimiza moja ya malengo ya tamasha hilo.
Msama alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za milipuko hiyo kwa Watanzania, na ndiyo maana wamejitolea kusaidia waathirika kwa misaada ya vyakula.
“Lengo kubwa la tamasha la Pasaka linaloratibiwa na Msama Promotions ni kusaidia watoto yatima na jamii kwa ujumla... hata hawa wenzetu walioathirika kwa kwa mabomu hatuna budi kuawasaidia.
"Natoa mwito kwa Watanzania wenzangu kuwa na moyo wa huruma na kuwasaidia waathirika hawa wa mabomu na pia nawa[pongeza Clouds FM kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha Watanzania kutoa misaada," alisema Msama.
Akipokea msaada huo, mtangazaji wa Clouds FM, Anthonio Nugazi anayeendesha kipindi cha Kambi Popote, alimshukuru Msama kwa kuonesha moyo wa kujitolea, na akatoa mwito kwa Watanzania wengine kuiga mfano.
Nugazi alisema Clouds 88.4 FM watawasilisha michango hiyo kwa wahusika katika kambi waliyoianzisha ya kutoa msaada Shule ya Msingi Mzambarauni iliyopo Ukonga, Mombasa, Dar es Salaam.
Tamasha la Pasaka la nyimbo za Injili za kumsifu Mungu, litafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Apili 24 mwaka huu na litashirikisha wasanii kutoka nchi sita za Afrika wakiwamo waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Lengo la tamasha la mwaka huu ni kupata fedha zitakazotumika kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane.
Milipuko hiyo iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha 511 KJ, iliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam, ilisababisha vifo vya watu 20 huku wengine zaidi ya 300 wakijeruhiwa.
Pia milipuko hiyo ilisababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi huku wengi wakipata hifadhi kwenye Uwanja wa Uhuru wakiwamo watoto wadogo waliopotezana na wazazi wao.

No comments:

Post a Comment