Saturday, June 27, 2015

JUMA NATURE AWAASA WASANII WANAOUTAKA UONGOZI WA KISIASA


Dar es Salaam. Msanii Juma Nature, ametoa rai kwa wasanii waliotangaza nia kuwania viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiwataka kusimama kwenye misingi ya kusaidia jamii badala na si vinginevyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nature ambaye mapema mwaka huu alifuta msimamo wake wa kutaka kugombea ubunge Jimbo la Temeke alioutangaza miaka mitatu iliyopita, alisema kwamba ni vyema wasanii wanaosaka nafasi za kisiasa kuzingatia watakayotakiwa kufanya kwa mujibu wa nafasi hizo za uwakilishi.
Nature alisema ni muhimu kufuata matakwa ya wananchi watakaowaongoza na kuacha kuweka mbele tamaa ya fedha kwa kuwa hayo siyo malengo ya uongozi wa kijamii bali huduma kwa wananchi.
“Kama wanaingia kwa ajili ya kwenda kwenye ubunge ni sawa, kwani wao ni watunzi wazuri wa zamani na uandishi wao upo kwenye jamii, lakini wasiende wakifikiria uongozi kuwa sehemu ya kujipatia fedha. Wawe karibu na wananchi watakaowaongoza kwa sababu hiyo ndiyo iliyo chini yao na inawategemea,” alisema Nature.
Kwa mujibu wa Nature ameamua kukaa pembeni kwa muda kutokana na utitiri wa wasanii walioweka wazi dhamira zao za kujiingiza katika siasa mwaka huu.
Alisema wazo hilo alilokuwa nalo muda mrefu, ameamua kujipa muda hadi ifikapo mwaka 2020 ili kuwaacha waliotangaza nia sasa kuendeleza mchakato huo.
“Mwenyezi Mungu akipenda ni tagombea mwaka 2020, nimeamua kwa mwaka huu niache mambo haya kwanza. Sasa nina kazi nyingi. Pili wasanii wengi wameshajitokeza, inatosha sana. Tusubiri tuone kwamba watafanya nini, ndipo na sisi tutaona nini tunafanya,” alisema Nature akiongeza kuwa kwa sasa yupo katika matengenezo ya video ya “Inaniuma Sana Remix” aliyomshirikisha Msaga Sumu.

No comments:

Post a Comment