Friday, September 17, 2010

BASATA LATOA DARASA KWA VIONGOZI WA WASANII.

Mmoja wa viongozi wa baraza la sanaa tanzania (BASAT) aiktoa muongozo kwa baadhi ya viongozi wa wasanii.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka viongozi wa mashirikisho ya wasanii kuhakikisha wanakuwa imara na thabiti ili kuleta ufanisi kwenye mashirikisho ya wasanii nchini yaliyoundwa na kupata viongozi wake hivi karibuni.
Hayo yamesisitizwa na Wakufunzi kutoka BASATA wakati wakitoa semina kwa viongozi wa mashirikisho ya wasanii nchini iliyofanyika wiki hii kwenye ukumbi wa Baraza hilo na kuhudhuriwa na viongozi wote wa mashirikisho ya wasanii na wajumbe wao.
Mashirikisho yaliyohusika kwenye semina hiyo ni pamoja na lile la Sanaa ya Muziki, Maonyesho,Ufundi na Filamu ambapo mada mbili zilizotolewa kwa viongozi hao ambazo ni Wajibu na Maadili ya Uongozi wa Mashirikisho ya Sanaa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji wa BASATA,Bw.Ruyembe Mulimba na na ile ya Mchakato wa Kuandaa Mpango Mkakati wa Shirikisho iliyowasilishwa na Mwalimu Rashid Masimbi kutoka Kituo cha Sanaa za Maonyesho Tanzania.
Akizungumza kwenye semina hiyo,Ruyembe alisema kwamba, viongozi wa mashirikisho ya wasanii hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wasanii,kuwa na mwenendo mwema, kuzingatia maadili ya uongozi, kuzingatia dhana ya kutangulia na kuelekeza huku mtangulizi akiwa anafahamu anakowapeleka watu anaowaongoza.
“Kiongozi mzuri lazima aelewe majukumu na mwenendo mwema katika kazi ya kusimamia watu ambao wanahusika na utendaji wa shughuli husika kwa ushirikiano na kwa pamoja kulingana na Katiba iliyopo” alisisitiza Ruyembe.
Aliongeza kwamba, historia inaonesha vyama vingi na shirika za wasanii zimekuwa kwenye migogoro isiyoisha kutokana na viongozi kutokuwa na utashi wa kuongoza., kutanguliza maslahi binafsi na kushindwa kabisa kuwa na maono ya kutekeleza mikakati inayokuwa imewekwa.
Alizidi kufafanua kwamba, wasanii wanakumbwa na changamoto nyingi sana zikiwemo za wao kuibiwa kazi zao, kunyonywa kupitia mikataba, kulipwa malipo kidogo na ukosefu wa masoko hivyo viongozi wa mashirikisho hawana budi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha changamoto hizo zinawekewa mikakati ya kupunguzwa kama si kumalizwa kabisa.
Naye Mwalimu Rashid Masimbi alisema kwamba, moja ya kazi ya viongozi hao wa mashirikisho ya wasanii ni kuhakikisha wanakuja na Mpango Mkakati wa muda mfupi na mrefu ambao utalenga kujenga dira ya utendaji na mafanikio ya mashirikisho.
Aliongeza kwamba, viongozi hawana budi kuwa na mpango mkakati ambao utaeleza nini kitafanyika,nani atakifanya, kwa namna gani na kwa muda gani.
“Mpango Mkakati ndiyo dira, dhamira, malengo, shughuli na matokeo ya utendaji wa shirikisho lolote hivyo lazima nyinyi viongozi mtuoneshe ni kwa jinsi gani tutayafikia haya” alisisitiza.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria semina hiyo waliishukuru BASATA kwa mpango huo na kusisitiza kwamba, semina kama hizo ziandaliwe mara kwa mara ili kujenga ufanisi wa mashirikisho ya wasanii na sekta ya sanaa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment