Friday, December 10, 2010

SHEREHE ZA UHURU ZILIVYOKUA JANA.

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika gari maalum na mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis Mwamunyange wakati akiwasili ndani ya Uwanja wa Uhuru jijini Dar leo.
Amir Jeshi Mkuu,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Gwaride leo katika maadhimisho ya miaka 49 ya Uhuru ndani ya Uwanja Uhuru,Jijini Dar leo.

NA MAGRETH KINABO- MAELEZO
RAIS Jakaya Kikwete leo aliuongoza umati wa Watanzania katika sherehe za miaka 49 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambapo alikuwa ni miongoni mwa watu walioshangiliwa katika sherehe hizo.

Ushangiliaji huo, ulionekana wakati Rais Kikwete alipoingia katika Uwanja wa Uhuru , alipokuwa akisalimia wananchi akiwa anazunguka uwajani hapo.

Sherehe hizo zilipambwa na mbwebwe ya watu mbalimbali walioonekana wakiwa na furaha na kushangilia viongozi waliokuwa wakiwasili katika uwanja huo.

Miongoni mwa viongozi walioshangiliwa ni Rais Mstaafu Serikali ya Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alishangiliwa na watu huku wakisema “mtoto wa mkulima’ , Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.

Mwingine ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar , Maalimu Seif Hamad , Mke wa Rais Mama Salma Kikwete , Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar , Balozi Seif Iddy ni miongoni mwa watu walioshangiliwa, wakati alipowasili uwanjani hapo.

Katika sherehe hizo viongozi wegine waliohudhuria ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Aman Abeid Karume na Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni, baadhi ya mawaziri , manaibu mawaziri, mabalozi , viongozi wa vyama vya siasa , majaji wakuu na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Sherehe hizo zilipambwa na gwaride maalum lililohusisha vikosi vya ulinzi na usalama ambalo lilishangiliwa, ikiwemo mizinga 21 aliyopingiwa Rais Kikwete , maonyesho ya ndege za kivita na ngoma za rirambi kutoka mkoa wa Mara.

Ngoma nyingine iliyokuwepo ni Sangula toka Morogoro na Gonga ya Zanzibar, likiwemo kundi la halaiki lililohusisha wanafunzi wa shule ya msingi 500 kutoka Tanzania Bara na 200 wa Zanzibar.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika sherehe hizo ni, ‘ Tudumishe Amani’.

Wakati huohuo, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO), Clement Mshana inasema Serikali inavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa gwaride zuri, kikundi cha halaiki , vikiwemo vya ngoma kwa umahiri wa burudani walizozitoa.

Pia imewapongeza wamiliki wa daladala na vyombo vingine vya usafiri kwa kuwawezesha wananchi kufika katika uwanja huo ili kuhudhuria sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment