b..

B1

Wynem

animation

Tuesday, November 27, 2012

SHARO MILIONEA KUZIKWA KESHO KIJIJINI KWAO LUSANGA, LUSHOTO.

Sharo milionea - enzi ya uhai wake

MSIBA wa msanii nyota wa uchekeshaji hapa nchini, Hussein Mkiety, maarufu kama 'Sharomilionea' umegusa hisia za wengi, huku King Majuto akikimbizwa Hospitali baada ya kushikwa na presha, hivyo kutishia usalama wake.
Mtoto wa King Majuto, Hamza Majuto, aliimbia HANDENI KWETU kuwa hali ya baba yake inaendelea vizuri kutokana na kuumizwa zaidi na msiba wa Sharomlionea anayetamba katika ulingo wa filamu na muziki hapa nchini.
Msanii huyo alikufa jana saa mbili za usiku Maguzoni, kilimita chache na kijijini kwao Lusanga, wilayani Muheza mkoani Tanga, baada ya gari lake alilokuwa akisafiria lenye namba za usajili T478 BVR Toyota Harrier kupinduka na kusababisha kifo chake.  
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe, alikiri kutokea kwa msiba huo na kusema kuwa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, Muheza, mkoani Tanga kwa taratibu za mazishi zinazopangwa na familia yake.
“Marehemu alikufa majira ya saa mbili za usiku kwenye barabara ya Segera alipokuwa anatoka Dar es Salaam kwenda Muheza, hivyo mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, huku gari lake likihifadhiwa pia kwasababu haliwezi kutembea,” alisema Masawe.
Taarifa za kifo cha msanii huyo aliyeibukia hivi karibuni na kufanya vema katika ulingo huo zilianza kuzagaa saa tatu za usiku, ikiwa ni dakika chache baada ya kufariki katika ajali hiyo ya kusikitisha kwa nyota huyo.
Katika mitandao yote ya kijamii kuanzia saa tatu za usiku zilizagaa habari zake, huku kila mmoja kiwa na hisia tofauti zilizotokana na madai ya kifo cha msanii huyo, ambaye baadaye jeshi la Polisi lilithibitisha kwa kupitia Kamanda wake, Masawe.
Sharomilionea ameshacheza filamu nyingi za uchekeshaji na kujipatia sifa kubwa, ikiwamo ile ya Sharo Millionea, Imekula Kwako, Jini Mahaba, Porojo na nyinginezo zinazofanya vyema katika tasnia ya filamu nchini.
Katika filamu ya Jini Mahaba, Sharomillionea anayetamba pia kwa msemo wake wa ‘Umebug Men’, anacheza kama mtu maarufu anayekwenda kujitambulisha kwa wake zake (Kingwendu) na kushangazwa na hali zao za maisha.
Sharomillionea anamshangaa mama yake mkwe anavyochambua mboga za majani wakati yeye sio utaratibu katika maisha yake. “Huyu ndio mama yako Men? Mbona anachambua majani,” aliuliza huku anakunja mdomo wake na kujifuta uso.
Maneno hayo yanamuumiza mama yake mkwe na kuamua kumuita mume wake (Kingwendu) na kuja kushangaa Sharobalo alivyokuwa katika mueneko wa super Star na kujikuta akipagawa alipoanza kukejeliwa na mkwe wake.
Mbali na filamu hiyo ya Jini Mahaba, mkali huyo pia ametamba katika filamu nyingi pamoja na nyimbo mbili alizorekodi, huku pia akililiwa na wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake, mara baada ya kuibuka kisanii.
Wasanii wengi waliozungumzia kifo cha Sharomillionea wakiongozwa na Steve Nyerere, walionyeshwa kuchanganyikiwa kwa msiba wa msanii aliyeanza kutokea peupe na kutamba mno katika sanaa ya uchekeshaji.
Sharomillionea aliyetokea katika ubavu wa nguli wa vichekesho nchini, King Majuto, anazikwa kesho Jumatano, kijijini kwao Lusanga, huku wasanii wengi wakitarajia kuhudhuria msiba na mazishi ya nyota huyo aliyeipenda pia nyumbani kwao Muheza.
Habari kwa Hisani ya Kambi Mbwana, Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment