Friday, September 21, 2012

SAKATA LA STUDIO YA JK LAIBUKA TENA

Sugu
Mwana FA
Amoss Makala
************************
Mwandishi Wetu

SIKU moja baada ya Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala kusema studio iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete ianze kufanya kazi katika nyumba ya kukuzia vipaji ya THT, Waziri Kivuli wa wizara hiyo, Joseph Mbilinyi 'Sugu' amemshangaa na kudai kuwa hayo ni maeneno yake binafsi na sio ya Serikali.
Sugu alisema kuwa Makala hajamshangaza tu yeye hata wabunge wenzake wa CCM akiwamo mwenyekiti Kamati ya bunge, Jenister Muhagama.
"Nikiwa kama Waziri Kivuli nimemshangaa sana Makala yeye ndio alisema juzi kwenye bunge la bajeti kuwa studio imemchafua sana rais hivyo kuna utaratibu unafanyika ili irudishwe kwenye mikono ya Basata na itumiwe na wasanii wote," alisema Sugu.
Alisema,"alipigiwa makofi mengi sana Bungeni, kuna nakala alinionyesha za maofisa wa Wizara zilizoonyesha mlolongo mzima wa utoaji wa studio umegubikwa na utata mkubwa na aliniahidi kulivalia njuga kikamilifu mpaka Muhagama akamsifu na kusema Makala kiboko, naamini hata yeye kama amemsikia Makala akisema tena studio ni ya THT atamshangaa."
Kauli ya Sugu imekuja siku moja baada ya Naibu Waziri huyo wa Habari kutembelea ofisi za THT zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuhoji studio hizo mahali zilipo na kuambiwa zimehifadhiwa Masaki.
"Mwana Fa vyombo vya studio vipo wapi?," aliuliza waziri Makala.
Mwana Fa, "Vipo Masaki vimehifadhiwa kutokana na utata uliotokea wa kina Sugu"
Makala alisema, "Hivyo vyombo vifungeni vianze kufanya kazi haviwezi tu kukaa siku zote hizo, vifungeni mvitumie ni vya kwenu hivyo mmepewa nyinyi na Rais, haiwezekani Rais akatoa studio kwa wasanii wote, mmesikia ni vya kwenu hivyo."
Lakini jana Sugu alisema atahakikisha analivalia njuga suala hilo hadi vifaa hivyo virudishwe Basata ili vinufaishe wasanii wote na kuhoji kuwa kilichombadilisha Makala msimamo wake ni kipi hadi kugeuka matamshi yake aliyoyatoa kwenye bunge la bajeti  lililomalizika siku za karibuni.
Akizungumzia suala hilo  Katibu Mkuu wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya (TUMA) Fredy Malik 'Mkoloni' alisema "Tunaamini alichokisema Makala ni kauli yake binafasi na si ya serikali hivyo haina mashiko, amesahau kabisa alichokizungumza bungeni, tunajipanga na kutoa tamko letu rasmi.

No comments:

Post a Comment