b..

B1

Wynem

animation

Friday, January 31, 2014

TAARIFA KUTOKA IKULU JUU YA UTEUZI WA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA.

 
Rais Jakaya Kikwete.

*****
Hatimaye, wajumbe 201 kutoka katika majina ya wawakilishi 2,722 wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini yaliyopelekwa Ikulu kwa ajili ya uteuzi wa Rais wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamepatikana.

Wajumbe hao wamepatikana baada ya kazi ya kuchambua majina hayo kufikia tamati.


Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu, aliliambia NIPASHE jana kuwa mchakato wa kuchambua majina hayo umefikia mwisho na sasa yatatangazwa wakati wowote kuanzia sasa.


“Process (mchakato) imefikia mwisho, wakati wowote (majina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walioteuliwa na Rais) yatatangazwa,” alisema Rweyemamu.

Jumatano wiki iliyopita, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema katika taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa Rais Jakaya Kikwete, anakusudia kukamilisha uteuzi wa wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mwanzoni mwa wiki ijayo.

Alisema baada ya uteuzi huo, majina hayo yatachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama kifungu cha 22 (3) cha Sheria iliyotajwa inavyomtaka kufanya.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapungua moja ya tatu ya wajumbe wote.

Wajumbe 20 watatoka kwenye mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na nusu yao watakuwa wanawake na moja ya tatu kutoka Zanzibar.

Wengine ni wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Vyama vya siasa 21 nchini, hivyo kila chama kitapeleka wajumbe wawili na mgawanyo utakuwa huo huo.

Wajumbe wengine na idadi yao kwenye mabano ni taasisi za elimu ya juu (20), makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowakilisha wavuvi (10) na vyama vya wakulima (20).

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na jumla ya wajumbe 635.

Kati ya wajumbe hao, wanaotoka katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini ni 201, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 358 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni 76.

Kati ya wajumbe 201 kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, nusu watakuwa wanawake na nusu nyingine watakuwa wanaume.
Wizara hiyo ilieleza kwamba wanawake watakuwa 101 na wanaume 100.

Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70, linatarajiwa kuanza rasmi katikati ya Februari, mwaka huu, kwa ajili ya kujadili na kuipitisha rasimu ya pili ya Katiba iliyopendekezwa.

Rasimu hiyo itawasilishwa katika Bunge hilo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Tayari Tume hiyo ilikwisha kuikabidhi rasimu hiyo kwa Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment