Wednesday, September 21, 2011

BASATA YAHIMIZA USAJILI WA KUMBI NA WASANII


 Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, BASATA Bw.Angelo Luhala (Kulia) akisisitiza jambo wakati akiongea na wasanii juu ya umuhimu wa wadau wa sanaa kujisajili kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu makao makuu ya Bara hilo. Alizungumzia pia ya haja ya wasanii kulinda haki zao. 
Mkuu wa Kitengo cha Matukio, BASATA Bw.Omary Mayanga (Kushoto) akizungumzia juu ya haja ya wasanii kuzingatia mikataba kwenye kazi zao katika Jukwaa la Sanaa Jumatatu wiki hii. Katikati ni Bw.Luhala na Kaimu Mratibu wa Jukwaa la Sanaa Bi. Agnes Kimwaga.
Mdau Kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akichangia mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wamiliki wa kumbi za burudani nchini kuhakisha wamezisajili huku likitoa wito kwa wasanii na wadau wa sanaa nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kujisajili.
Akizungumza kwenye programu ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa inayoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz), Mwenyekiti wa kamati ya usajili, BASATA Bw. Angelo Luhala alisema kwamba, kwa mujibu wa sheria suala la kujisajili ni la lazima.
“Naanzia kusema hapa, kila anayefanya kazi yoyote ya sanaa ni wajibu ajisajili, kujihusisha na shughuli za sanaa bila kujisajili ni kuvunja sheria,kanuni na taratibu za nchi” alisema Luhala.
Alizidi kueleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya nchi namba 23 ya mwaka 1984 Baraza limepewa mamlaka ya kusajili na kusimamia sekta ya sanaa nchini, hivyo mtu yeyote anayefanya shughuli za sanaa anapaswa kusajiliwa na kupewa kibali cha kufanya shughuli hizo.
Aliongeza kuwa, sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo kila anayefanya kazi ya sanaa hana budi kutambuliwa na serikali na Baraza kwa niaba ya serikali limepewa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Bwana Luhala wadau wanaopaswa kujisajili BASATA ni pamoja na wasanii wa fani zote, wakuzaji sanaa (mapromota), vikundi vya wasanii, kumbi zote za burudani, wafanyabiashara wa sanaa, vyama na asasi mbalimbali za sanaa.
Akizungumzia faida za kujisajili, Bw. Luhala alisema ni pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi, kutambuliwa na serikali, kupata utambulisho wa Baraza katika mahitaji mbalimbali, fursa za kushiriki maonyesho, taifa kuwa na takwimu sahihi za wadau wanaojihusisha na shughuli za sanaa na faida nyingine..
“Kuna watu wanajiuliza kwa nini wasajiliwe, lazima ieleweke kwamba, kila anayejihusisha na shughuli za sanaa lazima atambuliwe na serikali. Hapa ndipo tunapata takwimu pia” alisisitiza Bw. Luhala.
Wadau mbalimbali waliohudhuria programu hiyo walionekana kuwa na shauku kubwa kwani mbali na suala la usajili, Baraza lilitoa elimu kwa wasanii juu ya kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na wasanii kutakiwa kujisajili kwenye chombo kinacholinda Hakimiliki na shiriki cha Cosota.

No comments:

Post a Comment