
Rais Jakaya Kikwete
Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amempandisha cheo Mkuu wa Wilaya ya
Karatu, Daudi Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuwahamisha vituo
vya kazi wakuu wengine sita wa mikoa kuanzia jana.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
ilisema Ntibenda ataapishwa leo, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Wakuu wa mikoa waliohamishwa ni Elaston Mbwilo anayetoka Manyara kwenda
Simiyu kuchukua nafasi ya Paschal Mabiti aliyepewa likizo ya ugonjwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera anahamia Manyara kutoka Morogoro
na nafasi yake inachukuliwa Dk Rajabu Rutengwe kutoka Tanga alikokaa kwa
mwezi mmoja akitokea Katavi.
Magalula Magalula amehamishiwa Tanga kutoka Lindi ambako naye alikaa kwa
mwezi mmoja akitokea Geita na nafasi yake inazibwa na Mwantumu Mahiza
kutoka Pwani.
Mhandisi Evarist Ndiliko amehamishiwa Pwani kutoka Arusha alikohamia
hivi karibuni kutoka Mwanza.
Katika taarifa yake, Balozi Sefue alisema wakuu wengine wa mikoa
wanaendelea kubakia katika vituo vyao vya sasa vya kazi.
Uhamisho huo umekuja ikiwa ni mwezi mmoja kamili tangu Rais Kikwete
alipofanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa na kuwahamisha sita huku
wengine watatu wakipangiwa kazi nyingine.
Wakuu wa mikoa wanne wapya ni Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza
(Iringa), Halima Dendego (Mtwara) na John Mongella (Kagera).
Kabla ya kuteuliwa, Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mwanza;
Dk Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kilimanjaro na Mongela
alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Walioachwa kwa ajili ya kazi nyingine ni Dk Christine Ishengoma
(Iringa), Kanali Fabian Massawe (Kagera) na Kanali Joseph Simbakalia
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambaye tayari ameteuliwa kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo
ya Nje (EPZA).
Sorce- gazeti la Mwananch 08/12/2014
No comments:
Post a Comment