VIONGOZI wanne wa kundi la Uamsho wanaodaiwa kuhusika katika uchochezi wa vurugu za wiki iliyopita mjini zanzibar, jana walijisalimisha kwa makachero wa polisi na kuhojiwa kwa saa kadha kabla ya kuachiwa kwa masharti.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa habari mkuu wa Polisi Zanzibar, Mohammed Mhina ilisema viongozi hao ambao hakuwataja kwa majina walijisalimisha jana. Alisema viongozi hao pamoja na mpambe wao, walijisalimisha mapema asubuhi jana kwa viongozi wa polisi Mkoa wa Mjini Mangharibi Zanzibar waliwahoji kwa muda kabla ya kupelekwa Makao Makuu ya Upelelezi Zanzibar kwa mahojiano zaidi na baadaye kuachiliwa kwa dhamana.
Tangu kutokea kwa vurugu zilizosababisha kukamatwa kwa baadhi ya wafuasi wa kundi la Uamsho mjini Zanzibar na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao, viongozi hao watatu pamoja na mpambe wao walikuwa hawajapatikana.
Mara baada ya vurugu hizo za wiki iliyopita, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema polisi watahakikisha kuwa wale wote waliochochea vurugu hizo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa muda wa siku tatu, pia zilizosababisha kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na mali nyingine za madukani kuporwa na nyingine kuharibiwa na wafuasi wa kikundi hicho.
Mhina alisema polisi visiwani hapo wanaendelea kutoa wito kwa viongozi wengine walioshiriki katika vurugu hizo kujisalimisha wenyewe polisi badala ya kusubiri kutafutwa.
Hadi sasa watuhumiwa 78 wakiwamo viongozi wa kundi la Uamsho, wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo baadhi yao waliachiliwa kwa dhamana na wengine wakipelekwa rumande kwa kukosa wadhamini wenye kuaminika hadi Juni 11, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment