Philip Marmo
Na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Waziri wa Sera, na Uratibu waBunge katika awamu ya kwanza ya rais Jakaya Kikwete, Phillip Marmo amelisifia tamasha la Pasaka kwa kusema kwamba malengo yake ni mazuri kwani linasaidia jamii.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu litakalofanyika Aprili 24 lengo lake kubwa kwa mujibu wa Alex Msama ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ni kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wanawake wajane.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Marmo alisema kwamba amefarijika mno na muamko wa Msama Promotions waandaaji wa tamasha hilo kwa kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watoto yatima na wanawake wajane.
“Nimefarijika mno na muamko huu, kwakweli huu ni mfano wa kuigwa kwani ni watu wachache mno wanaoweza kuandaa matamasha kama haya na fedha zinazopatikana kuwasaidia watoto yatima na wajane,” alisema Marmo.
Aidha Marmo amesema kwamba kwa kiasi kikubwa tamasha hilo pia litasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kwani wengi hivi sasa wameamua kujikita katika muziki wa injili kwa ajili ya kumuimbia Mungu na kujipatia kipato.
“Unapokuwa na watu wenye uzalendo kama Msama Promotions kwa hakika kabisa vijana wengi watajitokeza na watahamasika kujiingiza katika muziki huu, kwani watakuwa na uhakika wa kujipatia kipato,” alisema Marmo.
Tamasha kubwa la Pasaka linatarajiwa kufanyika Aprili 24 mwaka huu siku ya sikuu ya Pasaka katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na baadaye kufanyika mjini Shinyanga Jumatatu ya Pasaka Aprili 25 na jijini Mwanza Aprili 26, lengo lake kubwa mwaka huu ni kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasiaid mtaji wa bishara wanawake wajane.
No comments:
Post a Comment