b..

B1

Wynem

animation

Tuesday, February 1, 2011

AY: WASANII TUGOMEE MALIO MADOGO KWENYE MAONYESHO.


Msanii wa kizazi kipya Ambwene Yessaya maarufu kwa jina la AY (Katikati) akiwasilisha mada kuhusu Harakati za kuufanya muziki wa Bongo Flava kuwa wa kimataifa mapema wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA.Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego na Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo , Godfrey Lebejo
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego (Aliyesimama) akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA.Katikati ni mwanamuziki wa kizazi kipya AY na Godfrey Lebejo ambaye ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo .
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maomyesho nchini, Agnes Lukanga akichangia hoja kwenye Jukwaa la Sanaa. Aliwataka wasanii kuwa na umoja katika suala la kupanga malipo katika maonyesho wanayoyafanya.
Sehemu ya wadau wapatao 165 waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA wiki hii.
Msanii wa mziki wa hip hop a.k.a bongofleva GETHOKING a.k.a SAIDAWG akifuatilia mada katia jukwaasnaaa

Na Mwandishi Wetu
Msanii anayepata mafanikio ya kimataifa katika muziki wa kizazi kipya hapa nchini Ambwene Yessaya aka AY amewataka wasanii kugoma kulipwa fedha kidogo kwenye maonyesho na badala yake wawe na msimamo mmoja katika kupanga viwango vya malipo yao .
AY aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Harakati za Kuufanya Muziki wa Kizazi kipya kuwa wa kimataifa kwenye Jukwaa la Sanaa linaofanyika kila wiki katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo alisema kwamba, wasanii hapa nchini wamekuwa ni wepesi kulalamika wanapolipwa malipo kidogo lakini wagumu kuchukua hatua katika kukomesha hali hiyo.
“Wasanii wengi wanalalamika malipo kidogo kwenye maonyesho, naona hali hii wanaitaka wenyewe. Kama msanii umeweka viwango vyako vya malipo na vinatambulika lazima anayekuhitaji atakulipa tu kazi kubwa inayobaki ni kuweka juhudi na ubunifu katika kazi tunazozifanya na kwenye maonyesho” alisema AY.
Alizidi kueleza kwamba, wasanii kwa pamoja wanao uwezo wa kukataa malipo wanayolipwa sasa kwenye maonyesho kwani wao ndiyo wenye kazi na ndiyo wanaoamua kuzitumia. Katika hili alisisitiza kwamba, ni bora msanii akubali kulala njaa kwa siku moja ili aweze kula kwa mwaka mzima badala ya ilivyo sasa ambapo wamekuwa ni wa kulilia fedha za kukidhi matatizo yao madogomadogo tu.
“Huko Nigeria kulikuwa na mchezo kama huu wa wasanii kulipwa fedha ndogo kwenye maonyesho lakini kuna siku wasanii wote waliamua kugoma kushiriki shoo za nyumbani hadi hali itakapobadilika. Leo hii msanii wa Nigeria analipwa dola laki moja na nusu hadi laki mbili wakati hapa kwetu ni ndoto” alisisitiza AY huku akiwaomba wasanii kuwa na umoja katika hili.
Wakati akiwasilisha mada yake, AY alitaja mambo kama uthubutu, kutengeneza kazi za sanaa zenye ubora, kujiamini, ushirikiano, kusimamia asili yetu na vitu vingine kama nguzo zitakazosaidia kuuvusha muziki wa kizazi kipya kwenye ngazi za kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA ambaye pia ni mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Ghonche Materego alisema kwamba, Baraza lake litaendelea kuwakutanisha wasanii wa hapa nchini na wadau wa sanaa kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuwapa fursa ya kujifunza kutoka kwao.
“Leo hapa tumeelezana masuala ya kujiamini, kuthubutu, kufanya kazi zenye ubora, haya yote ni ya msingi katika kukuza sanaa zetu. BASATA itaendelea kuwakutanisha wasanii na wadau wa sanaa kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kukuza sanaa zetu na kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ya Sanaa ni Kazi” alimalizia Materego.

No comments:

Post a Comment