Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristides Kwizela (Kushoto) akifuatilia burudani zilizokuwa zikitolewa na watoto wanaondaliwa na Baraza hilo kupitia programu ya ‘Sanaa kwa Watoto’ wakati wakitumbuiza kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii. Watoto hao wanatoka shule ya Msingi ya Msimbazi iliyoko Ilala jijini Dar es Salaam. Katikati ni Msanii wa filamu Honeymoon Mohamed na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Stadi za wasanii Bi. Vick Temu.
Sehemu ya watoto wanaoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia programu yake ya Sanaa kwa Watoto wakicheza igizo kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii. Watoto hao wanaosoma Shule ya Msingi Msimbazi walikuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa Sanaa.
Wasanii kutoka Kundi la Ngoma za Asili na Maigizo la Jivunie lenye makazi yake eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam wakionesha ufundi wao katika kuchenza ngoma za asili kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA linalofanyika makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba kwa mwezi mara mbili siku za Jumatatu.
Na Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wametakiwa kurejesha kwa jamii sehemu ya faida wanayoipata kupitia kazi zao za Sanaa kwa kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum ili kujijengea mtandao wa kudumu wa masoko, uhalali na taswira nzuri kwa jamii.
Wito huo umetolewa mapema wiki hii na mtengeneza filamu wa Tanzania mwenye makazi yake nchini Marekani Bi. Honeymoon Mohamed wakati akiwasilisha mada kuhusu Filamu za Kitanzania na Masoko kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
“Wasanii wanaitegemea jamii kama chanzo cha mapato yao hivyo ni lazima wajenge utamaduni wa kurejesha kile kidogo wanachokivuna kutoka kwa jamii kupitia kusaidia watu wenye uhitaji maalum” alisema Honeymoon ambaye filamu yake ya Daddy’s Wedding imeshinda tuzo kwenye tamasha la kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF) lililomalizika hivi karibuni eneo la Ngome Kongwe, Zanzibar.
Aliongeza kwamba watoto wenye uhitaji maalum wanapata faraja na kuhisi kupendwa na jamii pale wanapotembelewa mara kwa mara na watu mbalimbali wenye umaarufu na nafasi kubwa katika jamii hivyo wasanii wetu hawana budi kuwa sehemu ya kujenga faraja hii kwa watoto hawa.
Kwa mujibu wa Honeymoon wasanii wa Tanzania wako nyuma katika kuikumbuka jamii hususani kutembelea makazi ya watoto wenye uhitaji maalumu na kuchangia huduma mbalimbali zinazokuwa zinahitajika.
“Watoto wenye utindio wa ubongo wako wengi, kuna wale wenye ulemavu wa ngozi na wengine wanaishi wakiwa yatima kwenye vituo mbalimbali lakini wasanii wetu wamekuwa wazito kuwakumbuka. Wasanii hawana budi kuyakumbuka makundi haya maana wako kwa ajili ya jamii” alisisitiza.
Awali kabla ya uwasilishaji wa mada hiyo, watoto wanaoandaliwa kupitia programu ya BASATA ya ‘Sanaa kwa Watoto’ kutoka Shule ya Msingi wa Msimbazi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam walitoa burudani mbalimbali za Sanaa wakisaidiana na Kikundi cha Sanaa cha Jivunie chenye maskani yake neo la Mbagala Manispaa ya Temeke.
No comments:
Post a Comment