Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani , akiongea na waandishi wa habari
Waandishi wa habari wakimsikiliza kamanda wa polisi mkoa Mbeya
Na Mwandishi Wetu
POLISI Mkoani Mbeya, inawashikilia watu 13 wakiwemo viongozi wa Chama cha walimu na walimu wenyewe kwa tuhuma za kuhusika na vurugu zilizosababisha hasara zaidi ya shilingi milioni 100 wakati wa mgomo wa walimu ulioanza juzi.
Kitendo cha walimu hao kugoma kuingia darasani kilisababisha baadhi ya maeneo, wanafunzi kufanya maandamano ya amani ya kudai haki ya kufundishwa jambo ambalo linadaiwa kutumiwa vibaya na wahalifu kwani walitumia nafasi hiyo kufanya uhalifu kwa kuiba mali za watu.
Wahalifu hao walichoma ofisi za Halmashauri ya Mbozi ndani ya Mji mdogo wa Tunduma na kuiba mali zilizokuwemo kama kompyuta 5 za ofisi, pikipiki yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali.
Wahalifu hao walivunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka hiyo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani , aliwataja watuhumiwa hao wanaodaiwa kuhusika na uhalifu na kusababisha hasara ya shilingi milioni 117, 515,000 kuwa ni Mexon Mbilinyi, Akida Kondo, Chalres Rupia, Athumani Mgala, Stela Garbert, Atiliyo Benard, Nikodemus Exavely, Mashaka Amoni na James Kabuje.
Diwani, alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika na uhalibifu wa ofisi ya halmashauri ya mji mdogo wa tunduma ikiwa na kuiba mali yenye thamani zaidi ya milioni 100 na kwamba wote kwa pamoja wamefikishwa mahakamani leo.
Akizungumzia suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Aliwataja wahusika hao kuwa ni Mwalimu wa Patro Mangula na ni Katibu wa chama cha walimu wilaya ya Kyela ambapo inadaiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa akishirikiana na watu wengine kupita mashuleni kuhamasisha walimu waliokuwa wanaendelea na kazi ya kufundisha wajiunge na mgomo.
Wengine ni Mwalimu Emanuel Kyejo wa shule ya msingi Mbebe Wilaya ya Ileje na mjumbe wa chama cha walimu wilaya ya Ileje, Anyakingwe Lwinga na mjumbe wa chama cha walimu ambapo wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuhamasisha walimu kugoma.
Aidha, katika uhalifu wa Tunduma, Kamanada Diwani alisema kuwa polisi Mkoani Mbeya kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuokoa Mabati 168, Printa moja na mita mbili za maji, Bendera moja ya Taifa na photocopy mashine.
Pia, Kamanda Diwani alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi kwa nini askari wake walitumia Bomu na risasi katika vurugu hizo ambapo alisema kuwa Bomu hilo lilitumiwa kulitawanyisha kundi kubwa la watu lililokuwa linazidi kuelekea kwenye ofisi za serikali pamoja na Taasisi za kibenki na kwamba hakuna madhara yaliyojitokeza.
“Baadhi ya watu wamekuwa wakiipotosha jamii kuwa askari walitumia bomu kuwatawanya wanafunzi na ndio sababu za wananchi kuanzisha vurugu jambo hilo si kweli kwani bomu lilitumiwa baada ya kundi la wahuni lililokuwa likivamia ofisi na kuiba mali zilizomo ndani,”alisema.
Alisema, wakati kundi hilo linafanya vurugu tayari wanafunzi walikuwa wamerejea kwenye makao yao lakini kundi hilo la wahuni ndio lilikuwa likizidi kujikusanya na kuendelea kufanya uhalifu huo huku baadhi wakiwa wanaelekea kwenye eneo la Benki.
“Baada ya walinzi wa Benki kuona kundi hilo linaikaribia benki askari walipiga risasi mbili juu ili kuwatawanya na kwamba zoezi hilo lilisaidia kuwarudisha watu hao waliokuwa na lengo la kufanya uhalifu katika benki hiyo ,”alisema
Aidha, Diwani aliitaka jamii kuondoa mawazo potofu kwamba huenda vurugu hizo zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa jambo ambalo si kweli kwani jeshi la polisi linaamini kuwa kundi hilo la uhalifu halina itikadi yoyote ya siasa.
“Polisi inawashikilia watu hao kwa tuhuma za uhalifu na ninaamini watu hawa ni wahalifu hivyo watafikishwa mahakani kwa makosa ya uhalifu tu na wala hakuna siasa,”alisema
Hata hivyo aliwataka walimu pamoja na viongozi wa chama cha walimu kuacha kuwahamasisha wezao kufanya mgomo kwani wao tayari walitangaza kugoma na wamegoma hivyo kupita mashuleni na kuwakuta wezao wanafundisha na kuwalazimisha kugoma ni uvunjifu wa amani hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa zidi yao.
|
Tuesday, July 31, 2012
POLISI YAWASHIKILIA WATU 13 WAKIWEMO VIONGOZI WA CHAMA CHA WALIMU MKOANI MBEYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment