TAARIFA KWA UMMA
BAADA ya Watanzania wengi kutaka maoni ya Baraza la Wazee wa CHADEMA, juu ya uamuzi wa CCM, kupitia kwa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, kuwaondoa wazee, wakiwemo marais ambao waliwahi kuwa wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu, tumeonelea ni vyema kusema kama ifuatavyo.
Uamuzi huo wa CCM, ambao ni sehemu ya mabadiliko ya katiba ya chama hicho, mbali ya kuonekana kuwa umeiga namna CHADEMA inavyowatumia wazee, lakini uigaji huo bila shaka haukufanyika kwa makini kwa kuwa umewaengua kabisa katika nafasi ya maamuzi ya chama hicho wazee hao ambao ni makada waandamizi waliokitumikia chama hicho kwa muda mrefu.
Ndani ya CHADEMA, utaratibu wa kuwawezesha wazee kuunda Baraza la Ushauri, kwa nia ya kukishauri chama umeanza kutumika tangu mwaka 2006, pale baraza hilo lilipoundwa rasmi wakati wa mabadiliko ya katiba ya chama chetu makini.
Lakini pia kwa kutambua umuhimu wa wazee hao katika uendeshaji wa chama hiki, kikilenga kuwatumikia Watanzania, kwa kufanya maamuzi kwa kuangalia nchi inakotoka, ilipo na inakokwenda, wazee ndani ya CHADEMA wana nafasi katika vikao vya maamuzi ya chama.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA ni mjumbe wa Kamati kuu ya CHADEMA taifa; pia Wenyeviti wastaafu wa chama ni wajumbe wa kamati kuu ya chama taifa.
Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA ni mjumbe wa Sekretarieti ya chama. Pia yeye pamoja na mwenyekiti wa baraza hilo, wote ni wajumbe wa vikao vya Kamati Kuu. Kwa ujumla wazee wana uwakilishi kwenye vyombo vyote vya maamuzi vya chama kuanzia ngazi ya msingi, tawi mpaka ngazi ya taifa.
Hivyo mbali ya chama kupata ushauri wa wazee kupitia baraza la washauri hao kila inapohitajika, bado kinaweza kupata busara, hekima na uzoefu wao katika maamuzi mbalimbali ya chama yanayofanyika, kupitia vikao halali na muhimu.
Katika hali ya kawaida, wakati CCM inapita katika hali ngumu ya kisiasa, ikionesha kila dalili za kuchoka na mwisho wa kunyumbulika katika kuendelea kuendesha serikali, ilikuwa busara kuendelea kupata mawazo ya wazee katika vikao halali, badala ya kusubiri kuwaita na kuomba ushauri, wakati ambapo mambo yanakuwa yameshakwenda mrama.
Lakini pia CCM wasiwadanganye wananchi kuwa kwa namna ambavyo wamefikia tamati ya kuendelea kuaminiwa na Watanzania, kuwa eti wao wanaweza kusikiliza, kuamini na kufanyia kazi ushauri wa wazee hao, tena baada ya kuwaondoa katika vikao halali!
Tunasema hivyo tukikumbuka namna mapendekezo na ushauri wa iliyokuwa kamati ya Mzee Mwinyi, iliyoundwa kutatua matokeo ya mgogoro unaoendelea kukitafuna chama hicho, yalivyotelekezwa, huku chama kikikosa uwezo, umakini, uimara na uadilifu wa kuyafanyia kazi. Kwa sababu kinalinda maslahi ya ufisadi na mafisadi na kuwatosa Watanzania.
Lakini pia CCM waambie Watanzania, uamuzi huo, unasaidiaje Tanzania na Watanzania kwa ujumla kutoka katika mtanziko mkubwa wa matatizo yanayowakabili sasa, ikiwemo kuporomoka kwa uchumi na maisha kuzidi kuwa makali, yote yakisababishwa na uongozi mbovu wa chama hicho kilichoko madarakani kwa sasa.
Imetolewa jana tarehe 14 Februari;
Nyangaki Shilungushela
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CHADEMA