b..

B1

Wynem

animation

Wednesday, March 23, 2011

MASIKITIKO KWA AJALI ILIYOSABABISHA VIFO VYA WASANII WA KUNDI LA FIVE STAR MODERN TAARAB


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali iliyotokea Usiku wa Saa 2 Tarehe 21/02/2011 katika barabara kuu ya Iringa-Morogoro kwenye eneo la Hifadhi ya Wanyama ya Mikumi na kusababisha vifo vya watu 13 wakiwemo wasanii wa Kundi la Muziki la Five Stars Modern Taarab na kusababishwa wengine kadhaa kujeruhiwa.
BASATA linaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria. Kufiwa kwa wasanii hawa ni pengo kubwa kwa familia na Sekta ya sanaa nchini, kwani kupungukiwa na wasanii (wabunifu) 13 kumerudisha nyuma kimaendeleo sekta ya sanaa nchini na pengo hilo haliwezi kuzibika kwa njia yoyote iwayo.
Aidha,Baraza linawapa pole majeruhi na kuwaombea wapone haraka ili hatimaye waweze kurudi katika hali yao ya awali na kushiriki shughuli za sanaa.
Kwa tukio hili tunaungana na familia za wafiwa na wana Five Star Modern Taarabu kuwapa pole sana kwa msiba huu.Baraza linajua ni kipindi kigumu sana kwa wanafamilia na wadau wote wa Sanaa kwa Ujumla ingawa hatuna budi kuheshimu maamuzi ya Mungu kwani muda wote hayana makosa.
Baraza linatoa kiasi cha Tshs 500,000/= kama rambiwambi kwa Kundi la Five Star Modern Taarab ili zigawanywe kwa wafiwa na kusaidia shughuli mbalimbali za msiba huu mkubwa katika tasnia ya sanaa nchini.

Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi Amen

Ghonche Materego

KATIBU MTENDAJI

No comments:

Post a Comment